1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yemen: Wanaotaka kujitenga wadhibiti Aden

Angela Mdungu
29 Agosti 2019

Wapiganaji wanaotaka kujitenga nchini Yemen wameudhibiti tena mji mkuu wa muda wa nchi hiyo wa Aden ambao awali ulikuwa ukidhibitiwa na vikosi vya serikali ya Rais Abderabbo Mansour Hadi inayotambulika kimataifa

https://p.dw.com/p/3OgFS
Karte Jemen Sanaa Aden DE

Wapiganaji hao wameudhibiti mji huo baada ya mapigano na vikosi vya serikali ambavyo viliondoka katika mji huo wa bandari ya Kusini. Taarifa kutoka vyanzo cha usalama vya serikali ya Yemen zimethibitisha kuwa mji wa Aden sasa unadhibitiwa na wapiganaji hao na kwamba vikosi vya serikali ambavyo viliingia katika maeneo ya mji huo hapo jana vilijiondoa na kuelekea eneo jirani la Abyan.

Serikali ya Yemen inayotambulika kimataifa hapo jana Jumatano ilitangaza kuwa imepata tena udhibiti wa mji wa Aden kutoka kwa wapiganaji wanaotaka kujitenga ambao walikuwa wakiushikilia mji huo tangu Agosti 10 baada ya mapigano makali.

Kwa mujibu wa msemaji wa baraza la mpito la harakati za Uhuru la Kusini Haitham Nezar, vikosi vya wapiganaji hao wanaotaka kujitenga hivi sasa vinaitolea macho mikoa ya  Abyan na Shabwa ambayo imerejea tena mikononi mwa vikosi vya serikali tangu mapema wiki hii. Makamu wa Rais wa baraza la mpito la harakati za Uhuru la Kusini Hani bin Breik mapema leo aliandika kupitia ukurasa wake wa Twitter kuwa Aden iko salama.

Onyo latolewa kwa wafuasi watiifu kwa serikali

Bin Breik ameweka picha katika ukurasa wake zikimuonesha akiwa na viongozi wa eneo la Kusini, wakifanya ziara katika mitaa ya Aden ukiwemo uwanja wa ndege huku akiwaonya wafuasi watiifu kwa serikali kuwa wataadhibiwa.

Jemen Krieg STC-Kämpfer (Southern Transitional Council) in Aden | Mokhtar al-Noubi
Mkuu wa kikosi cha tano cha wapiganaji wanaotaka kujitenga wa Kusini mwa Yemen Mokhtar al-NoubiPicha: Getty Images/AFP

Kwa mujibu wa Bin Breik amesema wapiganaji wa vikosi vya Kusini vinavyopambana dhidi ya waasi wa Houthi wanaoshirikiana na Iran upande wa Kaskazini, waliitwa Kusini ili kushiriki mapambano. Breik amesema hawataendelea kupambana kulikomboa eneo la kaskazini kutoka kwa Wahouthi wakati Kaskazini yenyewe inawavamia.

Baraza la mpito la harakati za Uhuru la Kusini STC linapambana kulipatia uhuru eneo la Kusini mwa Yemen ambalo lilikuwa nchi huru kabla ya muungano na Kaskazini mnamo mwaka 1990. Mapambano kati ya vikosi vya usalama vya Kusini na vile vya serikali ambavyo kwa miaka mingi vimekuwa vikipigana kwa pamoja dhidi ya waasi wa kihouthi  yameongeza wasiwasi kwamba huenda nchi hiyo inayokabiliwa na njaa ikasambaratika.