Yemen: Saudi Arabia yatangaza hatua ya kusimamisha mapigano
9 Aprili 2020Msemaji wa jeshi la Saudi Arabia Kanali Turki al-Maliki ameeleza katika tamko rasmi kuwa muda wa kusimamisha mapigano utachukua wiki mbili, kuitikia wito uliotolewa na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres wa kutaka mapigano katika migogoro yote duniani yasimamishwe katika juhudi za kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.
Msemaji huyo wa jeshi la Saudi Arabia amesema muda huo unaweza kurefushwa ili kuziwezesha pande zote zinazohusika na mgogoro wa nchini Yemen kujadili hatua za kufikia suluhisho endelevu katika mgogoro huo. Hata hivyo mpaka sasa viongozi wa waasi wa Kihouthi bado hawajatoa jibu juu ya tangazo la Saudi Arabia.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambaye hivi karibuni alitoa wito wa kusimamisha mapigano katika migogoro yote duniani ameunga mkono tangazo la Saudi Arabia na amesema hatua hiyo inaweza kusaidia kuendeleza juhudi za kuleta amani na kupambana na janga la maambukizi ya virusi vya Corona.
Guterres ameitaka serikali ya Yemen inayoungwa mkono na majeshi yanayoongozwa na Saudi Arabia pamoja na waasi wa Kihouthi wazingatie wajibu wao, wasimamishe mapigano mara moja na waanze mazungumzo chini ya upatanishi wa mjumbe wa Umoja wa Mataifa bila ya kuweka masharti.
Hata hivyo muda mfupi tu baada ya Saudi Arabia kutoa tamko juu ya kusimamisha mapigano wakaazi wa mji unaopiganiwa wa Marib walisema kwamba mji wao ulishambuliwa kwa kombora linalotuhimiwa kuwa la waasi wa Kihouthi.
Mshauri wa rais wa Yemen Abdel -Malek al-Mekhlafi amewalaumu waasi hao kwa kufanya shambulio hilo. Amesema shambulio hilo linaonyesha kuwa waasi hao wanakoleza vita badala ya amani. Watu zaidi ya 270 waliuawa kutokana na mapigano makali kati ya majeshi ya serikali ya Yemen yanayosaidiwa na Saudi Arabia na waasi wa Kihouthi yaliyotokea katika siku10 zilizopita.
Pande hizo mbili zinalipigania jimbo muhimu la mpakani la Jawf na pia jimbo la kati la Marib lenye utajiri wa mafuta. Mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu yameilaumu Saudi Arabia juu ya mgogoro wa nchini Yemen ambao umesababisha vifo vya watu wengi. Watu zaidi ya laki moja wamekufa kutokana na mgogoro huo ambao pia umesababisha maafa makubwa kwa mamilioni ya watu kutokana na uhaba wa chakula na huduma za afya.
Vyanzo:/AP/DPA