1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yemen: Majeshi ya ardhini yapelekwe kupambana na waasi

7 Mei 2015

Serikali ya Yemen imeiomba jumuiya ya kimataifa kuingilia kati haraka mzozo wa nchi hiyo kwa lengo la kuisaidia kupambana na waasi wa Houthi, wanaopigana na vikosi vinavyomtii Rais Abed-Rabbo Mansour Hadi.

https://p.dw.com/p/1FM20
Majeshi ya muungano unaoongozwa na Saudi Arabia, yakiwa Yemen
Majeshi ya muungano unaoongozwa na Saudi Arabia, yakiwa YemenPicha: picture-alliance/AP Photo/H. Jamali,

Katika barua iliyoandikwa na Balozi wa Yemen kwenye Umoja wa Mataifa, Khaled Alyemany, kwenda kwa baraza la usalama la umoja huo, Yemen imeomba majeshi ya ardhini kuingilia kati mzozo wa nchi hiyo, hasa katika miji ya Aden na Tais.

Alyemany amesema vikosi vya ardhini vitasaidia kuiokoa nchi hiyo kutoka mikononi mwa waasi ambao wamekuwa wakilengwa na mashambulizi ya anga na vikosi vya muungano wa kijeshi unaoongoozwa na Saudi Arabia.

Barua hiyo iliyotumwa jana kwa rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lenye wanachama 15, Yemen pia imeyaomba mashirika ya kimataifa ya haki za binaadamu kuweka kumbukumbu za ukiukwaji wa haki za binaadamu na ukatili unaofanywa dhidi ya watu wasioweza kujitetea.

Wito wa kupelekwa vikosi vya ardhini umetolewa wakati ambapo jumuiya ya kimataifa badala yake, inataka mapigano yasitishwe mara moja ili kuweza kusambaza misaada ya kibinaadamu kwa watu walioathiriwa na mapigano hayo.

Rais Abed-Rabbo Mansour Hadi
Rais Abed-Rabbo Mansour HadiPicha: Getty Images/S. Gallup

Saudi Arabia imesema inafikiria kusitisha kwa muda mashambulizi ya anga ili kuruhusu misaada kuingizwa Yemen. Jana Jumatano, watu 32 wameripotiwa kuuawa wakati wakijaribu kuukimbia mji wa kusini wa Aden kwa kutumia njia ya baharini.

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen kuzungumza na Hadi

Leo, mjumbe mpya wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen, Ismail Ould Cheick Ahmed, anatarajiwa kufanya mazungumzo na Rais Abed-Rabbo Mansour Hadi, kwenye mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh. Ziara hiyo inalenga kuanzisha tena mazungumzo ya kuutatua mzozo huo kwa njia za kisiasa. Hadi anaishi uhamishoni nchini Saudi Arabia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Yemen, Reyad Yassin Abdulla, ametoa wito wa jitihada kufanyika ili kuwasambaratisha waasi wa Houthi pamoja na wapiganaji wanaoumuunga mkono rais wa zamani wa nchi hiyo, Ali Abdullah Saleh, ambao wanafanya mauaji makubwa.

'' Tunauomba muungano wa kijeshi ufanye kila linalowezekana, tena haraka iwezekanavyo kuwaangamiza waasi wa Houthi na wanamgambo wa Saleh na kuukoa mji wa Aden na watu wake pamoja na Wayemen wote kwa ujumla,'' alisema Abdulla.

Aidha, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, jana amewasili Riyadh, pia akijaribu kutafuta suluhu ya mzozo wa Yemen, na anatarajiwa kukutana na Mwanamfalme Mohammed bin Nayef pamoja na Mfalme Salman.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John KerryPicha: Reuters/A. Harnik

Kerry anatarajiwa kushinikiza kusitishwa mashambulizi ili raia waweze kupata misaada ya kibinaadamu. Akizungumza wakati yuko nchini Djibouti, Kerry alisema ana wasiwasi sana kuhusu hali ya kibinaadamu inayojitokeza nchini Yemen.

Umoja wa Mataifa umesema kiasi raia 600 wameuawa tangu muungano wa kijeshi wa Saudi Arabia uanze mashambulizi dhidi ya waasi mwezi Machi mwaka huu na wengine 300,000 hawana makaazi.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,APE
Mhariri:Iddi Ssessanga