Yemen katikati ya mkwamo
24 Februari 2015Jioni ya jana ilimalizika kwa kwa mripuko wa bomu karibu na chuo cha kijeshi mjini Sanaa, ambacho kiko kwenye ngome kuu ya waasi wa jamii ya Houthi wanaoudhibiti mji huo mkuu tangu mwezi Septemba 2014.
Hakuna ripoti za majeruhi wala waliouawa kutokana na mashambulizi hayo, ambayo yanaashiria namna gani waasi wa Houthi wanavyopambana na upinzani mkali kutoka kwa jamii na makundi mengine nchini humo.
Hakuna kundi lililodai kuhusika na mashambulizi hayo hadi sasa, ingawa inafahamika kuwa mfumo wa kiusalama umeporomoka kabisa nchini Yemen, huku kundi la waasi wa Kisunni wanaojinasibisha na al-Qaida, likitumia nafasi hiyo kuendeleza machafuko. Kundi hilo limehusika na mashambulizi kadhaa kama hayo huko nyuma dhidi ya jamii ya Houthi, ambalo linawachukulia kuwa si Waislamu safi.
Mripuko huo ulitanguliwa na maandamano ya maelfu ya watu waliojitokeza kuunga mkono tangazo la Rais Mansour Hadi kurejea madarakani.
Waandamanaji pia walitaka waasi wa Houthi kuachia udhibiti wa taasisi na majengo makuu ya serikali na kuelekea kwenye meza ya mazungumzo.
"Tumeshiriki kwenye maandamano haya kuonesha uungaji mkono wetu kwa uhalali wa kikatiba unaowakilishwa na Rais Abd-Rabbu Mansour Hadi, ambaye ndiye rais pekee halali wa Yemen, na pia tumeshiriki ili kukataa ghasia na utegemezi wa matumizi ya nguvu," alisema Abdulwali'i Salim, mmoja wa waandamanaji hao.
Hadi arejea madarakani
Juzi Jumapili, Rais Hadi alitangaza kurejea kwenye nafasi yake kama mkuu wa nchi, akionekana kwenye mkanda wa vidio akifanya mkutano wake wa kwanza na maafisa wa serikali tangu kutoroka kizuizi cha nyumbani siku ya Jumamosi na kukimbilia kwenye mji mkuu wa iliyokuwa Jamhuri ya Yemen Kusini, Aden.
Hadi alikuwa ametangaza kujiuzulu mwezi uliopita (Januari 2015) kufuatia shinikizo la waasi wa Houthi, ambao wanashikilia kasri ya rais sambamba na taasisi kadhaa muhimu za serikali.
Msaidizi wa Rais Hadi ameliambia shirika la habari la AFP kwamba rais huyo alituma barua rasmi kwa bunge kufuta tangazo lake la kujiuzulu, akisema kwamba hatua ya waasi wa Houthi kushikilia madaraka ni kinyume cha sheria na batili.
Bado hakujawa na kauli yoyote kutoka uongozi wa waasi wa Houthi, ambao mapema wiki iliyopita ulikubaliana na wapinzani wao kuunda baraza la mpito kuelekea uchaguzi na katiba mpya, lakini wachambuzi wa mambo wanahofia kwamba sasa Yemen inaelekea kuwa dola isiyotawalika katika Ghuba ya Arabuni, mithali ya Somalia kwenye Pembe ya Afrika.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Josephat Charo