Huu ndio wakati wa Afrika kufahamu ukweli
3 Desemba 2018Kulingana na Nafo nchi za Afrika ndizo zinazochangia kidogo kwenye mabadiliko ya tabia nchi lakini ndizo zinazoathirika pakubwa. Bara hilo tayari linakabiliwa na ukame, kiwango kikubwa cha mvua na mafuriko huku athari zikiwa mbaya zaidi.
Kwa kutegemea nchi yenyewe, athari za tabia nchi zinaleta uharibifu wa kati ya asilimia tano na kumi ya kiwango jumla cha pato la nchi. Umoja wa Mataifa umeonya kwamba Afrika bado inakabiliwa na hali mabaya zaidi, huku ikitarajiwa kwamba kufikia mwaka 2020, hadi watu milioni 250 watakuwa wanakabiliwa na tatizo kubwa la maji kutokana na ongezeko la kiwango cha joto.
Mtu wa kawaida haoni umuhimu wa yanayojadiliwa mikutano ya COP
Umoja wa Mataifa unasema iwapo ongezeko hilo litakuwa zaidi ya nyuzi mbili, nusu ya Waafrika wote watakabiliwa na utapia mlo.
Nnimmo Bassey ni mwanaharakati wa mazingira kutoka Nigeria.
"Mtu wa kawaida haoni umuhimu wa yanayojadiliwa katika mikutano ya COP, watu wanaona athari zenyewe za ongezeko la joto duniani, mabadiliko ya hali ya hewa, watu wanaona changamoto za uzalishaji wa chakula na watu wana wasiwasi sana wanataka jambo lifanyike," alisema Bassey.
Lakini mkutano huu wa COP 24 unatarajiwa kuleta mabadiliko. Ni katika mkutano huu ambapo sheria za kina zinatarajiwa kuzingatiwa ili kutimiza lengo muhimu zaidi la mkutano wa uliofanyika Paris mwaka 2015 ambapo ilikubaliwa kwamba kiwango cha joto duniani kipunguzwe kwa nyuzi 1.5 ikiwezekana.
Mambo ni lazima yabadilike katika mkutano huu
Wataalam wanaonya hatua zilizochukuliwa na jamii ya kimataifa kufikia sasa hazitoshi na wanataka kuwepo na sheria kali zitakazoheshimiwa na kila mmoja. Zaidi ya hayo wawakilishi wa Afrika katika mkutano huo wanalenga kuona iwapo ahadi iliyotolewa na nchi tajiri duniani katika mkutano wa Paris, ya kuzisaidia nchi maskini kwa kuzilipa dola bilioni 100 kuanzia mwaka 2020 itatimia. Ahadi hiyo ilikuwa ni ya kuzisaidia nchi maskini kuweza kukabiliana na athari za tabia nchi.
Mwanaharakati Bassey anasema ni sharti mambo yabadilike katika mkutano huu.
"Ninataraji tu kwamba mkutano huu utakuwa jukwaa ambapo wawakilishi wataanza kuzungumza kutoka moyoni mwao na sio tu kutokana na masuala ya kisiasa, iwapo hilo halitofanyika, utakuwa tu mkutano mwengine wa COP," alisema Bassey.
Mwandishi: Daniel Pelz
Tafsiri: Jacob Safari
Mhariri: Iddi Ssessanga