Yanayojiri Hong Kong: Maalfu ya watu waendelea kuandamana
5 Agosti 2019Kwa mara nyingine polisi walitumia gesi ya kutoa machozi ili kuwakabili waandamanaji waliojazana kwenye sehemu za burudani na za umma kwenye viwanja vya wilaya kadhaa za jiji la Hong Kong. Gesi hiyo ya machozi ilitupwa kutoka juu kwenye majengo ya ghorofa. Polisi pia waliwafyatulia waandamanaji risasi za mpira.
Kiongozi wa jiji la Hong Kong Carrie Lam amewataka waaandamanaji waache kufanya vurumai. Lam ametoa wito huo katika hotuba yake ya kwanza baada ya kunyamaza kimya kwa siku kadhaa. Wakati maandamano yakiendelea katika muktadha wa mgomo mkuu, polisi imesema watu 82 wamekamatwa. Na wakati huo huo serikali kuu ya China mjini Beijing imetumia maneno makali katika tahariri iliyosomwa kwenye televisheni ya taifa, kusema kwamba vurumai haipaswi kuendeleakatika jiji la Hong Kong.
Mgomo huo mkuu uliilenga hasa sekta ya usafiri wa umma, leoikiwa ni siku ya kazi. Kwa mujibu wa taarifa sehemu saba za njia za reli zilifungwa leo asubuhi, wakati wa pilika pilika kubwa za watu kwenda makazini. Njia za reli zipatazo saba zilifungwa kutokana na waandamanaji kuzuia milango ya kuingia kwenye vituo vya treni. Safari za ndege zaidi ya 200 zilivunjwa kwenye uwanja wa ndege wa Hong Kong na hali kama hiyo ilikumba stesheni za treni za mwendo kasi ambazo shughuli zake zilisimama. Idadi kubwa ya wafanyakazi wa uwanja wa ndege waliripoti kuwa wagonjwa ili kupata sababu ya kushiriki katika mgomo.
Maandamano ya leo kwenye wilaya saba za jiji la jiji la Hong Kong yamefanyika baada ya waanadamanaji kupambana na polisi wa kuzuia fujo mwishoni mwa wiki iliyopita. Msemaji wa polisi amefahamisha kwamba wapinzani 420 wameshakamatwa tangu tarahe 9 mwezi juni siku ambapo watu zaidi ya milioni moja walihamasika kushiriki kwenye maandamano ya kupinga mswada wa sheria wa kuiwezesha serikali ya mamlaka ya ndani ya Hongkong kuwapeleka wahalifu China ili kuhukumiwa.
Kiongozi wa jiji la Hong Kong, Carrie Lam, amesema maandamano yamesababisha taharuki miongoni mwa wananchi na ameahidi kuwa serikali yake itasimama imara katika juhudi za kurejesha na kudumisha utulivu ili kuweza kurejesha imani. Wakati huo huo, mkuu wa kitengo cha habari kwenye polisi ya Hong Kong, ameeleza kuwa polisi inaungwa mkono na serikali ya Hong Kong kwa nia moja, na kwa hivyo hapatakuwa na haja ya kuwaleta wanajeshi kutoka China ili kurejesha utulivu.
Vyanzo:/AFP/AP/https://p.dw.com/p/3NLEw