1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yanayoendelea nchini Ujerumani baada ya uchaguzi

29 Septemba 2017

Viongozi wawili wa chama cha mrengo mkali wa kulia cha Afd, Frauke Petry na mumewe Marcus Pretzel waliojitoa kwenye chama hicho wanapanga kuanzisha chama kitakachokuwa mpinzani wa chama cha mrengo mkali wa kulia cha AfD.

https://p.dw.com/p/2krRq
Deutschland Frauke Petry und Marcus Pretzell in Berlin
Picha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

Frauke Petry na mumewe Marcus Pretzel walijitoa kutoka chama cha Afd wamesema hatua yao inalenga kuanzisha kundi jipya ndani ya bunge na baadaye wanatarajia kuunda chama kipya kwa ajili ya kukipinga chama hicho chenye mrengo mkali wa kulia ambacho wanakilaumu kwa kuzingatia msimamo wa kibaguzi uliopitiliza. Petry, aliondoka kutoka kwenye mkutano na waandishi wa habari wa viongozi wa chama hicho mjini Berlin uliofanyika baada ya uchaguzi. Viongozi wengine watatu wa AfD walikuwa Mwenyekiti Alexander Gauland, Alice Weidel mwenyekiti mwenza wa chama hicho na Jörg Meuthen. Petri alisema chama hicho cha AfD kinahitaji kufuata njia za kawaida na za kweli, kwani kwa sasa mtazamo wa chama hicho unaunda kuwa upinzani usiofaa.

Deutschland Bundestagswahl Merkel PK
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Reuters/F. Bensch

Wakati huo huo chama cha Kansela Angela Merkel kimechukua hatua yake ya kwanza ya kukishawishi chama cha Kiliberali cha FDP.  Chama hicho hakikuwakilishwa bungeni kwa muda wa miaka minne iliyopita baada kushindwa kupata asilimia tano katika uchaguzi wa mwaka 2013. Kwingineko chama cha SPD ambacho kitakuwa chama kikubwa cha upinzani katika bunge la taifa Bundestag kimemchagua kiongozi wake wake atakayekiongoza chama hicho bungeni ambaye ni Bi Andrea Nahles aliyekuwa waziri wa ajira katika serikali iliyopita. Nahles atakuwa mwanamke wa kwanza kuongoza chama cha upinzani bungeni hatua inayoonekana kuwa ni muhimu kwa ajili ya kujiimarisha kwa chama Social Democratic SPD.

Kwa upande wa kimataifa rais wa Israel Reuven Rivlin amekilaumu chama cha mrengo mkali wa kulia cha AfD cha nchini Ujerumani na ambacho kimeingia bungeni kwa mara yake ya kwanza. Rais Rivlin amesema jamii ya Wayahudi nchini Ujerumani ina wasiwasi mkubwa. Amempongeza kansela Angela Merkel kwa kupinga waziwazi makundi yanayolemea siasa za mrengo mkali wa kulia.

Naye waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu katika mazungumzo kwa njia ya simu na kansela Merkel hakukitaja chama hicho cha AfD moja kwa moja bali alilaani matamshi dhidi ya Wayahudi yanayotolewa na makundi yenye mitazamo mikali.

Mwandishi: Zainab Aziz/DPAE/dw.com/p/2kq89 / dw.com/p/2knZS

Mhariri:Josephat Charo