Wulff atoa wito wa uvumilivu wa kidini
20 Oktoba 2010Ankara.
Rais wa Ujerumani Christian Wulff ametoa wito wa uvumilivu zaidi wa kidini katika hotuba yake katika bunge la Uturuki . Katika hotuba yake mjini Ankara , ikiwa ya kwanza kwa kiongozi wa taifa kutoka Ujerumani, Wulff amesema kuwa ni muhimu kuruhusu waumini wa dini ambao ni wachache nchini Uturuki na Ujerumani kuabudu dini zao. Wulff pia ametumia hotuba hiyo ya kihistoria kusifu ushirikiano baina ya nchi hizo mbili, na kushughulikia mjadala unaoendelea nchini Ujerumani kuhusiana na ujumuisho wa Waturuki. Amesisitiza kuwa wahamiaji wa Kituruki ni sehemu ya Ujerumani, na kwamba hawana haja ya kupoteza utambulisho wao. Ameongeza hata hivyo, kuwa kuna matatizo mengi yanayokabili ujumuisho wao. Ametoa wito kwa wahamiaji wote wa Kituruki kujifunza Kijerumani, kufuata sheria muhimu, na kukubali maadili ya kuishi ya Kijerumani.