Wolfsburg au B.Munich -Berlin au Stuttgart kutwaa ubingwa ?
15 Mei 2009Kinyanganyiro cha taji la ubingwa wa Ujerumani kinapamba moto jumamosi hii huku timu 4 zikiania taji hilo kileleni-Wolfsburg,Munich,Berlin na Stuttgart.
Katika Premier League-Ligi ya Uingereza, kocha wa Arsenal, Arsene Wenger alisema kabla ya changamoto na Manchester united kuwa, siri ya mafanikio ya Sir Alex ni kiu chake cha kukusanya vikombe-
Duru ya 4 ya kombe la klabu bingwa barani Afrika inarudi uwanjani kwa mabingwa mara 6 Al Ahly wakiwa na miadi na Santos ya Angola mjini Cairo.
Bingwa wa Olimpik na wa rekodi za dunia mjamaica Usain Bolt, kukimbia kesho mita 150 mjini Manchester, Uingereza.
Armin Veh aliyeitawaza Stuttgart mabingwa miaka 2 nyuma, atakuwa kocha mpya wa viongozi wa Bundesliga-Wolfsburg msimu ujao. Hii imetangazwa ijumaa kabla Wolfsburg inayoongoza Ligi kwa magoli 2, kuteremka uwanjani kupambana na Hannover.
Wolfsburg inabidi kuwa na kocha mpya baada ya kocha wao wa sasa aliewaongoza kileleni mwa Bundesliga, Felix Magath kuamua kuhamia Schalke msimu ujao.
Jarida la dimba "KICKER-liliarifu kwamba miongoni mwa makocha wengine waliozingatiwa na Wolfsburg ambayo huenda ikaibuka mabingwa msimu huu mradi imetamba leo mbele ya Hannover, ni pamoja na kocha wa zamani wa schalke Mirko Slomka, kocha wa sasa wa Hamburg Martin Jol na Christoph Daum wa FC Cologne.
Hapo kabla, mabingwa Bayern Munich walitangaza kumuajiri mdachi Van Gaal kuanzia Julai mwaka huu kujaza pengo lililoachwa na Jurgen Klinsmann alietimuliwa baada ya kupigwa kumbo Munich nje ya champions league na kombe la Taifa la Ujerumani.
Timu 4 ziko kileleni mwa Bundesliga huku yakisalia mapambano 2 tu kumtawaza bingwa: Wolfsburg, Munich, Hertha Berlin na Stuttgart. Munich na Wolfsburg kila moja ina pointi 63 kwa 62 za Berlin na 61 za Stuttgart. Atakaeteleza leo ataachwa nyuma katika mbio hizi za ubingwa:
Wanaoongoza kwa mabao mengi katika kinyanganyiro cha Kombe la Afrika la klabu bingwa ni Ahmed Abdelmalek wa Harras al-Hadoud ya Misri pamoja na Timothy Mbewe wa Red Arrows ya Zambia alietia mabao 5. Wanafuatwa nafasi ya pili na Lassina Bamba wa SO Armee ya Ivory Coast pamoja na Manucho Barros wa Santos ya Angola. Wao wametia mabao 4. Nafasi ya 3 wanafuata Lamouri Djediat na Abdelmalik Ziaya wa Setif ya Algeria.
Riadha:Bingwa mara 3 wa olimpik Usain Bolt wa Jamaiaca, ataingia mitaani kesho huko Manchester kukimbia mbio za masafa ya mita 150 zinazokumbusha mbio kama hizo zilizokimbiwa karne ya 19 nchini Uingereza.
Bolt ni mwanariadha maarufu wakati huu akiwa bingwa wa Olimpik wa Beijing katika masafa ya mita 100-mita 200 na mita 100X4 kupokezana. Bolt atapewa changamoto na wanariadha 2 wa kingereza Mark Lewis-Francis na Simeon Williamson. Bolt shabiki wa dimba wa manchester united anaepiga kambi yake Uingereza wakati wa msimu wa riadha barani Ulaya, asema hizo zitakuwa mbio zake za kwanza mjini Manchester.
1977 waandaji wa riadha waliandaa changamoto ya mbio za mita 150 kati ya Donovan Baily na Michael Johnson kuamua nani ana mkasi zaidi. Bailey alikuwa bingwa wa Olimpik wa 1996 mjini Atlanta na wa rekodi ya dunia wakati Johnson alikuwa bingwa wa rekodi ya mita 200. Mbio hizo zikamalizika kwa muda wa sekunde 8 baada ya Johnson kuumia. Baada ya mashindano ya olimpik ya Beijing mwaka jana, hakuna shaka nani ni mwanariadha wa kasi ulimwenguni. Usain Bolt wa Jamaiaca.
Muandishi:Ramadhan Ali/RTRE
Mhariri: Josephat Charo