Wizara ya fedha yashambuliwa Yemen
29 Novemba 2017Bomu hilo lililipuka nje ya jengo la wizara ya fedha, mjini Aden, ambako ni makao makuu ya muda ya serikali ya Yemen, inayoungwa mkono na Saudi Arabia na inayotambulika na jumuiya ya kimataifa.
Taarifa zilizoripotiwa na shirika la habari la AP zinasema baadhi ya maafisa na watu walioshuhudia zinasema bomu hilo kubwa lililotegwa kwenye gari limeliharibu jengo hilo la serikali na kusababisha vifo vya watu watano na wengine 12 kujeruhiwa.
Hata hivyo, duru za kiusalama zimearifu kwamba, kundi la wanamgambo linalojiita Dola la Kiislamu, IS limedai kufanya shambulizi hilo kwenye jengo hilo, na kusababisha vifo vya walinzi wawili na wengine wanne kujeruhiwa.
Kwenye taarifa kupitia tawi lake la propaganda la Amaq, wanamgambo wa IS wamedai kulipua bomu hilo lililotegwa kwenye gari lililokuwa limeegeshwa nje ya jengo la wizara ya fedha.
Taarifa zilizotolewa na taasisi moja binafsi ya habari ya Aden al-Ghad majengo sita ya ghorofa yaliharibiwa vibaya na mlipuko wa bomu hilo, likiangazia shuhuda zilizotolewa na wakazi wa eneo hilo. Mlipuko huo ulivunja vioo vya madirisha na makazi jirani, taarifa hiyo iliongeza.
Shambulizi hilo linalodaiwa kufanya na kundi la wanamgambo wa IS, ni la pili kufanywa na kundi hilo la itikadi kali katika mji wa Aden mwezi huu.
Hapo jana kwenye mkutano wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa unaozungumzia ugaidi, unaofanyika makao makuu ya Umoja huo, Afisa mwandamizi kwenye ofisi ya katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa inayoshughulikia vita dhidi ya ugaidi Vladimir Voronkov, ametoa mwito wa kuongezwa kwa ushirikiano baina ya mataifa na kubadilishana taarifa ili kukabiliana na mitandao ya kigaidi.
Novemba 5, wanamgambo hao walisema walihusika na mashambulizi mawili yaliyofanyika wakati mmoja katika idara ya usalama ya mjini Aden, yaliyosababisha vifo vya takriban wanajeshi saba.
Mji huo wa Aden umeshuhudia wimbi la mashambulizi katika miezi ya hivi karibuni, na hususan yakilenga vikosi vya usalama, maafisa wa serikali na wanasiasa, na kusababisha vifo vya mamia. Baadhi ya mashambulizi hayo yalidaiwa kufanywa na IS na mengine na Al-Qaeda.
Tangu mwaka 2014, Yemen, ambayo ni moja kati ya mataifa maskini zaidi za Kiarabu, imekabiliwa na machafuko makubwa kati ya serikali inayoungwa mkono na Saudi Arabi na waasi wa Houthi ambao ni washirika wa Iran. Waasi wa Houthi bado wanaudhibiti mji mkuu wa Yemen, Sanaa na maeneo mengine ya nchi hiyo, pamoja na mashambulizi yaliyoanzishwa na jeshi chini ya uongozi wa Saudi Arabia Machi 25, 2015, dhidi yao.
Pengo la kimamlaka limesababisha wapiganaji wa jihadi wa Al-Qaeda na wapinzani wao IS kuimarisha uwepo wao nchini Yemen, na hususan katika eneo la kusini linalodhibitiwa na serikali.
Huku wakiungwa mkono na Marekani, vikosi vinavyoongozwa na Saudi Arabia vimeongeza kampeni yake nchini Yemen, ya kukabilina na wapiganaji wa jihadi katika eneo hilo la Kusini, lakini bado wanadhibiti baadhi ya maeneo ya milimani na kwenye jangwa.
mwandishi: Lilian Mtono/AP/AFPE/DPAE
Mhariri: Josephat Charo