Wizara 12 zachukuliwa na vyama vya upinzani Afrika Kusini
1 Julai 2024Chama Kiukuu cha Upinzani nchini humo cha Demokratic Alliance DA, kitachukua viti sita, huku kiongozi wa chama hicho John Steenhuisen akitangazwa kuongoza wizara ya kilimo.
Chama tawala cha ANC kimechukua wizara 20, ikiwa ni pamoja na wizara nyeti kama vile Wizara ya Mambo ya Nje, Wizara ya Ulinzi, Wizara ya Nishati na Fedha.
Baraza hilo ambalo lina wizara 32, linatajwa kuwa ni kubwa zaidi likiwa na ongezeko la wizara mbili, ikilinganishwa na miaka iliopita.
Soma pia:Rais Ramaphosa hatimaye ateua baraza jipya la mawaziri
Akihutubia katika televisheni ya taifa Ramaphosa amesema serikali mpya ya mseto imejizatiti katika kuleta mabadiliko ya kweli kwa Waafrika Kusini.
"Katika siku hii tumeunganisha nguvu zetu kwa pamoja, Tumeungana kama Waafrika Kusini, tukiwa na matumaini makubwa." Alimesema Rais Ramaphosa.
Aliongeza kwamba "tuchukue tumaini hili, ili kila mmoja wetu aweze kuunganisha nguvu katika kuijenga Afrika Kusini ya ndoto yetu."
Vipaumbele vya serikali mpya ya Afrika Kusini
Serikali hii mpya ambayo kwa mara ya kwanza katika historia ya taifa hilo la kusini mwa Afrika, imeundwa na vyama 11, inatarajiwa kuongoza taifa hilo ambalo linauchumi imara zaidi barani humo.
Chama cha ANC cha Ramaphosa kilipoteza wingi wa viti kwenye Bunge kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 30, katika uchaguzi wa Mei 29 na kupoteza hadhi ya kuongoza serikali peke yake.
Serikali hii mpya inayojumuisha vyama vya upinzani imepanga kutoa kipaumbele katika masuala kadhaa muhimu, ikiwemo ukuaji wa uchumi, haki za kijamii kadhalika kustawisha demokrasia ya nchi.
Soma pia:Chama cha MK chajiunga na muungano wa upinzani Afrika Kusini
Kupambana na umaskini, ukosefu wa ajira, na uhalifu pia ni miongoni mwa vipaumbele, pamoja na kushughulikia rushwa na unyonyaji wa serikali ambao umekuwa ukilalamikiwa na wakaazi wa taifa hilo.
Ikumbukwe kwamba muungano huo wa uongozi umeundwa bila makubaliano yoyote ya muungano thabiti. Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wametilia shaka uthabiti na ufanisi wa aina hiyo ya serikali.
Taifa la Afrika Kusini limezidi kuwa muhimu katika medani za kimataifa kutokana na nafasi yake ya kijografia kwenye bara la Afrika, ambalo ni tajiri kwa malighafi zinazohitajika kuelekea matumizi ya nishati safi.
Taifa hilo pia ni mwanachama pekee kutoka barani Afrika katika kundi la mataifa 20 yaliyostawi na yanazoinukia kwa kasi kiuchumi duniani G20.