1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wito watolewa kwa mataifa ya umoja wa Ulaya kusitisha biashara na Israel kupinga ukiukaji wa haki za binadamu katika mamlaka ya Palestina.

Sekione Kitojo2 Septemba 2007

Biashara kati ya umoja wa Ulaya na Israel inapaswa kusitishwa kama njia ya kupinga vitendo vinavyokwenda kinyume na haki za binadamu katika maeneo ya Wapalestina, hayo yamesemwa katika mkutano wa umoja wa mataifa.

https://p.dw.com/p/CH8b

Chini ya kile kinachotajwa kuwa ni makubaliano ya ushirika , Israel kwa hivi sasa inafaidika na biashara huru katika bidhaa za viwandani, pamoja na upendeleo maalum kwa bidhaa za kilimo zinazoingia katika mataifa ya umoja wa Ulaya.

Luisa Morgantini, makamu wa rais wa bunge la Ulaya , amesema kuwa taasisi yake imetoa wito wa makubaliano haya kusitishwa. Hadi sasa, hata hivyo, miito hiyo imepuuziwa na serikali za mataifa ya umoja huo pamoja na watendaji wa umoja wa Ulaya, halmashauri ya Ulaya.

Hii ni licha ya waraka wa pili wa makubaliano, ambao ulianza kutumika mwaka 2000 , unaotaka pande zote kuheshimu haki za binadamu.

Morgantini alikuwa akizungumza katika mkutano wa umoja wa mataifa kuhusiana na mzozo kati ya Israel na Palestina mjini Brussels uliofanyika August 30-31.

Amedai kuwa umoja wa Ulaya umefanya makosa mengi katika kushughulikia uhusiano wake na mataifa ya mashariki ya kati , hususan katika mwaka uliopita.

Ilikuwa si sahihi, amesema, kwa umoja huo kusitisha misaada ya moja kwa moja katika mamlaka ya Palestina mwaka 2006, wakati chama chenye misingi ya dini ya Kiislamu cha Hamas kilipopata ushindi katika uchaguzi wa bunge ambao maafisa wa umoja huo wanauona kuwa ulikuwa wa haki na wakidemokrasia.

Ameshutumu , pia , uamuzi wa umoja wa Ulaya wa kulenga misaada yake katika eneo la ukingo wa magharibi kuliko Gaza. Kama raia wa Ulaya , tunapaswa kuendeleza na sio kugawa lakini kuwaunganisha watu wa Palestina, amesema. Sera yetu baadhi ya nyakati ni kinyume chake ameongeza.

Ameeleza wasi wasi wake juu ya jinsi umoja wa Ulaya tangu mwaka 2005 unavyoendesha ujumbe wa unaosaidia katika udhibiti wa mpaka katika eneo la Rafah, eneo pekee ambao linaunganisha eneo la Gaza na sehemu nyingine duniani.

Kivuko hicho cha mpakani kwa kiasi kikubwa kimefungwa na majeshi ya Israel tangu Hamas kuchukua madaraka ya ukanda wa Gaza mwezi Juni, huku wafanyakazi wa umoja wa Ulaya wanaohusika katika ujumbe huo hawachukui hatua yoyote kuondoa vikwazo vya kutokutembea watakako Wapalestina.

Eoin Murray kutoka shirika la Ireland linalopambana dhidi ya umasikini Trocare, amesema kuwa umoja wa Ulaya umekuwa mshirika mwenza wa Israel katika kuikalia Palestina na kwamba ujumbe wa umoja wa Ulaya katika kivuko cha Rafah unapaswa kufutwa.

Kila asubuhi , ameliambia shirika la habari la IPS, kuwa wajumbe katika ujumbe wa umoja wa Ulaya huenda hadi mahali hapo katika kivuko hicho ambacho kinajulikana kama Karim Abu Salam kwa Wapalestina na Kerin Shalom kwa Waisrael. Waisraeli husema kuwa hawawezi kwenda hapo kutokana na sababu za kiusalama na wafanyakazi wa umoja wa Ulaya wanakubaliana nao. Kufungua kivuko cha Rafah ni muhimu ili kufungua mawazo ya watu na kumaliza kibano kinachowakumba watu wa Gaza. Kwa hivi sasa , iwapo mtu ana ugonjwa wa saratani katika ukanda wa Gaza atakufa tu kwasababu Waisrael hawatamruhusu kuvuka kwenda Misr kwa ajili ya matibabu.

Murray ameutaka umoja wa Ulaya kufikiri upya kuhusu nia walioionyesha ya kufanyia ukarabati miundo mbinu, ikiwa ni pamoja na shule na mahospitali, ambayo yameharibiwa na Israel.

Umoja wa Ulaya umekadiria kuwa uharibifu wa kiasi cha Euro milioni 44 umefanywa na Israel katika miradi iliyogharamiwa na umoja wa Ulaya katika mamlaka ya Palestina.

Richard Kuper , msemaji wa taasisi ya European Jews for a Just Peace, Wayahudi walioko Ulaya wanaopigania amani na haki , taasisi yenye makao yake makuu mjini London, amedai kuwa Israel imekwenda kinyume na mkataba wa nne wa Geneva, uliokubalika mwaka 1949, ambao unatoa haki kwa watu walioko katika uvamizi na kukaliwa na taifa la nje.

Amedai kuwa Israel imepata upendeleo maalum na umoja wa Ulaya na Marekani kuliko mataifa mengine katika eneo hilo, Israel imeruhusiwa kuwa na silaha za kinuklia na haitawajibishwa kwa kupuuzia maazimio kadha ya umoja wa mataifa.