1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wingu la majivu ya volcano kuathiri mazishi ya rais wa Poland.

16 Aprili 2010

Hii inatokana na kufutwa kwa safari kadhaa za ndege barani Ulaya kufuatia kusambaa kwa wingu hilo la majivu.

https://p.dw.com/p/MyhC
Wingu la majivu ya volcano nchini Iceland.Picha: AP

Wingu la jivu la volkano ambayo inayotabiriwa kuendelea kuripuka katika siku zijazo sasa huenda likaathiri mazishi ya Rais wa Poland Lech Kaczynski yanayotarajiwa kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali duniani akiwemo rais wa Marekani Barack Obama mnamo Jumapili hii.

Msaidizi katika ofisi ya rais nchini humo ameeleza kwamba familia za marehemu zinataka mazishi yaendelee kama kawaida katika eneo la Krakow huku maafisa wa ngazi za juu wakisubiriwa kufanya uamuzi wa mwisho baadaye hii leo.

Maafisa nchini humo hapo awali walipanga kuusafirisha mwili wa marehemu hadi Krakow kwa ibada hiyo ya mazishi katika kanisa la mji huo la Wawel siku ya Jumapilli  baada ya misa ya maombi huko Warsaw hapo kesho Jumamosi.

Mbali na rais huyo wa Marekani, mwenziwe wa Urusi, Dmitry Medvedev, Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, Rais wa Ufaransa, Nicholas Sarkozy, Mwanamfalme Charles wa Uingereza na viongozi wengine wengi wanatarajiwa kuhudhuria mazishi hayo.

Rais wa nchi ya Slovakia, Ivan Gasparovic, inaarifiwa anatazamiwa kusafiri kwa gari hadi huko Krakow kufuatia  kufungwa kwa viwanja vyote vya ndege nchini mwake hii leo hadi siku hiyo ya Jumapili.

Kinyume na hapo awali ambapo uwanja wa Krakow ulikuwa wazi na uliotarajiwa kutumika na viongozi mbalimbali duniani watakaowasili kwa mazishi ya Rais huyo, sasa uwanja huo umefungwa pamoja na viwanja vingine vya ndege nchini humo. Hivyo basi Poland sasa imejumuika katika orodha ya nchi ambazo zimefunga viwanja vyake vya ndege kutokana na wingu hilo la majivu linaloendelea kusambaa.

Wingu hilo la majivu linalotokea kwenye mripuko wa volkano kilomita 120 kutoka eneo la kusini mashariki mwa mji mkuu wa Iceland, Reykjavik, linaendelea kusambaa katika anga za bara la Ulaya huku wataalam wakiarifu hatari ya kuendelea kwa mirupuko mingine ya volkano katika siku zijazo. 

kwa mujibu wa msemaji wa shirika la usalama wa anga nchini Ujerumani Kristina Kelek ni vigumu kubaini ukweli kuhusu wingu hilo la jivu. Bibi Kelek alisema,''bado tunaendelea kuangalia mwenendo wa wingu hili na kwa sasa hatuwezi kusema chochote kiukamilifu''.

Msemaji wa wizara ya maswala ya nchi za nje nchini Iceland, Urdur Gudmundsdotir ameeleza kwamba barabara kadhaa ziliharibika pamoja na vizuizi vya kuingia katika baadhi ya mashamba katika eneo hilo. Shughuli ya kuwahamisha watu kutoka eneo hilo ingali inaendelea huku msemaji huyo akidokeza kuwa watu kati ya 40 na 50 wanatarajiwa kuhamishwa watakao kuwa miongoni mwa watu takriban 800 kutoka eneo hilo la mkasa waliohamishwa wiki hii.

Huku hayo yakijiri shirika la afya ulimwenguni, WHO, limetangaza kuathirika kwa watu walio na matatizo ya kupumua kutokana na  wingu hilo la jivu.

Msemaji wa shirika hilo, Daniel Epstein, amesema kwamba bado hazijaorodheshwa athari zenyewe, lakini athari iliyopo iwapo majivu hayo yatatuwa kwenye ardhi basi ni hatari kwa afya za wanadamu.

Mripuko huo mkubwa wa volkeno hiyo nchini Iceland ni wa tano tangu kutulia kwa Iceland katika karne ya 19.

Mwandishi :Maryam Abdalla/RTRE/APE

Mhariri:Josephat Charo