WINDHOEK : Pohamba aonya juu ya mapinduzi kwa suala la ardhi
19 Machi 2005Rais mteule wa Namibia Hifikepunye Pohamba hapo jana ameonya kwamba nchi yake hiyo ya kusini mwa Afrika inaweza kukabiliwa na mapinduzi venginevyo wakulima wa kizungu wanakubali kuitowa ardhi yao.
Akizungumza katika hafla ya kumuaga katika wizara yake ya ardhi ambayo ataiwacha ili kuchukuwa hatamu za uongozi kutoka kwa Rais wa muda mrefu Sam Nujoma hapo Jumaatatu Pohamba amewataka wakulima wa biashara kukubali pendekezo la serikali la kununuwa ardhi yao.
Pohamba amekaririwa akisema hatua hiyo ya kuchukuwa ardhi yao haimaanishi kutaifishwa bali ina maanisha kuiuzia ardhi serikali kwa bei muafaka kama inavyotajwa na katiba na sheria ziliopo.Ameongeza kusema kwamba hadi hii leo hakuna ardhi yoyote ile iliyochukuliwa.
Rais huyo mteule ameonya kwamba subira miongoni mwa wazalendo walio wengi nchini Namibia inafikia kikomo.
Takriban wakulima 3,800 ambao wengi wao ni wazungu wanamiliki asilimia 44 ya ardhi inayolimika katika nchi hiyo kame yenye idadi ya watu milioni 1.82 (milioni moja laki nane na ushee)