Wimbledon : Miaka 77 ya Uingereza kusubiri yamalizika
8 Julai 2013Sauti zilipazwa, na shangwe zilikuwa zinaongezeka kila wakati, kila point iliyokuwa inapatikana ambayo ilikuwa inamchukua Andy Murray karibu na kumaliza miaka 77 ya Uingereza kusubiri kulinyakua taji la Wimbledon.
Ndiyo hali inayoweza kuelezewa katika mchezo wa tennis uliofanyika jana kati ya Andy Murray wa Uingereza na Novak Djokovic wa Serbia , ambapo mashabiki 15,000 walishuhudia patashika nguo kuchanika katika fainali iliyodumu karibu saa tatu na nusu na hatimaye kwa mara ya kwanza katika muda wa miaka 77 Uingereza umeweza kuonja raha ya kuwa mabingwa tena katika mchezo huo.
Mafanikio ya Grand slam hayakuja kirahisi ana haraka kwa Andy Murray katika muda wake wa kucheza tennis, na hakika hayakuja kwa haraka Uingereza katika uwanja wao wenye sifa tele na pia mashindano hayo maarufu duniani ya Wimbledon. Kwa hiyo kulikuwa na kitu kinachoendana na mchezo huo jana , hamasa ikiongezeka, wasi wasi , shauku na kila aina ya mvuto kwa Waingereza kusubiri muda zaidi kuweza kutawazwa mabingwa wa taji hilo.
Andy Murray ambaye yuko katika nafasi ya pili katika orodha ya wachezaji bora wa mchezo wa tennis duniani kwa wanaume, amemshinda mchezaji nambari moja Novak Djokovic kwa seti 3-0 , kwa michezo 6-4 , 7-5 na 6-4.
Andy Murray amesema haikuwa rahisi kama ilivyoonekana:
"Nilifanyakazi ya ziada katika mchezo ule. Ni points chache ambazo nimezipata kwa taabu sana katika mchezo kama huo katika maisha yangu. Ulikuwa mchezo tofauti kabisa ukilinganisha na mashindamno ya US open na kushinda ubingwa wa Wimbledon. Ndio ... kwa kweli bado sijaamini, nashindwa kuweka kichwa changu sawa nikifikiri kuhusu mchezo huo. Siamini."
Naye Novak Djoklovic alimwagia sifa tele Murray kwa ushindi wake jana.
"Ukweli ni kwamba alicheza vizuri sana katika wakati muafaka. Nilikuwa katika seti ya pili na ya tatu , mbele kwa 4-2 na kupoteza mipira ya kuanzia katika mchezo huo na nilimruhusu kunipita bila sababu maalum. Alipata ushindi katika kila mchezo na alikimbilia kila mpira na kuupata. Alikuwa kila mahali katika eneo lake na alionesha mchezo wa hali ya juu wa tennis. Bila shaka yoyote, alistahili kushinda."
Baadhi ya mashabiki wa mchezo huo wanasema kuwa mchezo wa tennis sasa unarejea katika hadhi yake na shauku, baada ya kudorora kidogo.
Jumamosi Wajerumani walikuwa katika runinga zao wakikodolea macho mchezo wa tennis kati ya kijana chipukizi Sabine Lisicki na Marion Bartoli wa Ufaransa : Katika mchezo huo Marion Bartoli aliibuka mshindi kwa seti 2-0 , kwa michezo 6-1 na 6-4.
Nao Daniel Nestor na Kristina Mladenovic waliibuka kidedea baada ya kushinda pambano dhidi ya Bruno Soares na Lisa Raymond kwa seti 2-1 kwa michezo 5-7 6-2 na 8-7 kwa wachezaji wawili wawili wanaume na wanawake jana katika mashindano hayo ya Wimbledon.
Wizara kuchunguza madai ya wachezaji
Wizara ya michezo nchini Nigeria imeunda jopo la kuchunguza mzozo wa wachezaji wa timu ya taifa ya nchi hiyo ambao karibu usababishe kuvurugika kwa mashindano ya kombe la mabara nchini Brazil kwa timu hiyo kujitoa, baada ya wachezaji kugoma kutoka katika hoteli waliyofikia nchini Namibia wakitakiwa kusafiri kwenda Brazil.
Wizara hiyo imesema jopo la watu sita limeundwa na litaanza kazi siku ya Alhamis na kuripoti kuhusu uchunguzi wao katika muda wa wiki mbili.
Wachezaji wa Nigeria waligoma kwenda katika mashindano ya kombe la mabara mwezi uliopita baada ya malipo yao ya ziada , "bonasi", kwa ajili ya michuano ya kufuzu kucheza katika fainali za kombe la dunia kupunguzwa na shirikisho la soka la Nigeria kutoka kitita cha dola 10,000 iwapo timu hiyo itapata ushindi hadi dola 5,000 na dola 2,500 iwapo itatoka sare.
Wizara ya michezo iliingilia kati na kutoa fedha za ziada , na kusafisha njia kwa kikosi hicho cha tai wa kijani wa Nigeria kusafiri kwenda Brazil, ambako waliwasili muda mfupi tu kabla ya mashindano hayo kuanza.
Rais wa FIFA Sepp Blatter amewaambia viongozi wa michezo wa Palestina jana kuwa atazungumza na maafisa wa Israel wajaribu kupunguza adha za kusafiri kwa wachezaji wa soka wa Palestina. Blatter alikuwa anatarajiwa kukutana na viongozi wa chama cha soka nchini Israel leo na alikuwa anatarajia kuzungumza na viongozi wa kisiasa nchini humo kuhusu suala hilo.
Wapalestina wamekasirishwa na ukweli kwamba majeshi ya usalama ya Israel , ambayo yanadhibiti matembezi ya watu kati ya ukanda wa Gaza na maeneo yanayokaliwa na Israel ya ukingo wa magharibi wanawazuwia wachezaji kusafiri kama watakavyo kati ya maeneo hayo yaliyotengwa.
Ghana yaingia nusu fainali
Ghana imefanikiwa kuingia katika nusu fainali ya mashindano ya vijana chini ya miaka 20 inayofanyika nchini Uturuki baada ya kuishinda Chile kwa mabao 4-3 jana.
Ghana ambayo ni taifa la kwanza kutoka bara la Afrika kutawazwa mabingwa wa kombe hilo la vijana chini ya miaka 20 itakutana na Ufaransa katika nusu fainali wakati Iraq ilifanikiwa kuingia katika hatua hiyo baada ya kuitoa Korea ya kusini kwa mikwaju ya penalti baada ya kutoka sare ya mabao 3-3 dhidi ya Korea ya kusini. Iraq sasa itakwaana na Uruguay katika nusu fainali ya pili.
Wakati huo huo mashindano ya kitaifa ya vijana wa umri wa miaka 17 imemalizika mwishoni mwa juma hili nchini Tanzania, ambapo mkoa wa Mwanza umeibuka mabingwa wa mashindano hayo kwa kuishinda Morogoro kwa bao 1-0 katika mchezo uliofanyika katika uwanja wa Kumbukumbu ya Karume jijini Dar Es Salaam.
Nayo timu ya Kinondoni ilitwaa taji la wanawake kwa kuifunga Ilala kwa bao 1-0.
Wachezaji wanaohama
Kwa upande wa wachezaji kuhama na kuingia katika vilabu vipya msimu ujao, Olympique Lyon imepata saini ya mlinzi wa pembeni raia wa Ureno Hugo Miguel Lopes kwa kuazimwa kutoka Sporting Lisbon.
Mchezaji wa zamani ambaye aliwahi kuwa mchezaji bora wa mwaka katika bara la Ulaya Hristo Stoichkov amejiuzulu kuwa kocha wa timu ya CSKA Sofia ya Bulgaria baada ya kuwa katika wadhifa huo kwa muda wa mwezi mmoja, akisema kuwa hana imani na wamiliki wa klabu hiyo pamoja na udanganyifu wao usio kwisha.
Mlinzi wa zamani wa timu ya taifa ya Ufaransa Eric Abidal amejiunga na Monaco kwa mkataba wa mwaka mmoja baada ya mkataba wake na Barcelona kumalizika.
Nyota wa soka wa zamani wa Ufaransa Thierry Henry atakuwa miongoni mwa wachezaji 10 waliotajwa jana katika kikosi cha ligi ya Marekani , Major League Soccer all-stars kitakachopambana na AS Roma ya Italia Julai 31 mjini Kansas.
Mbio za magari.
Iwapo washindani wake wanatataka kumzuwia Sebastian Vettel kushinda ubingwa wake wa nne mfululizo katika mbio za magari za formula one,watahitaji kutafuta mbinu mbabada. Vettel alishinda jana mbio hizo za Grand Prix nchini Ujerumani na kuwaacha washindani wake kwa zaidi ya point 34 dhidi ya Fernando Alonso anayeendesha gari ya Ferrari.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / ape / rtre
Mhariri: Mohammed Khelef