Wimbi la mashambulio laendelea Nigeria
24 Januari 2012Mapigano ya asubuhi ya leo, yalizuka baada ya kiasi ya miripuko 15 kutokea katika eneo lililo karibu na kituo cha polisi. Milio ya risasi iliendelea kusikika hata baada ya miripuko hiyo kusita. Mashahidi wamesema, hadi watu 2 wameuawa asubuhi ya leo, baada ya vikosi vya usalama kuizingira nyumba iliyoshukiwa kutumiwa kama maficho ya wanamgambo wa kundi la Kiislamu la Boko Haram.
Hapo jana, polisi walifanikiwa kuzuia mashambulio, baada ya kugundua magari 10 yaliyotegwa mabomu na miripuko mingine, katika mji wa Kano ulio wa pili kwa ukubwa nchini Nigeria. Mkuu wa polisi Ibrahim Idris amesema, raia 150, polisi 29 na maafisa wengine 6 wameuawa katika mashambulio ya Ijumaa katika mji huo wa Kano ulio na wakaazi milioni 4.2 wengi wao wakiwa ni Waislamu.
Rais wa nchi hiyo, Goodluck Jonathan ameahidi kuimarisha usalama huku akipambana na mzozo mbaya kabisa tangu kushika madaraka miezi tisa iliyopita, wakati wimbi la machafuko likizidi nchini humo na kundi la Boko Haram likilaumiwa kwa ghasia hizo. Desemba 31, Jonathan alitangaza hali ya hatari katika baadhi ya maeneo ya kaskazini, kufuatia wimbi la mashambulio. Kundi la Boko Haram limetuhumiwa kuhusika na mashambulio hayo vile vile.
Mshindi wa zawadi ya uandishi sanifu ya Nobel, Wole Soyinka aliewahi kuonya juu ya hatari ya kuibuka vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo, sasa ametoa mwito kwa Wanigeria wenzake, kutolipizana kisasi. Hata viongozi wa kisiasa wanajaribu kuhakikisha kuwa machafuko ya hivi sasa, hayatochochea mzozo mkubwa zaidi, katika nchi hiyo ambako Waislamu wengi huishi kaskazini mwa nchi wakati eneo la kusini likiwa na Wakristo zaidi.
Wakati huo huo, mtu aliedai kuwa msemaji wa Boko Haram, amesema, wamefanya mashambulio hayo kwa sababu serikali, imekataa kuwaachilia wanachama wenzao walio kizuizini. Inaaminiwa kuwa baadhi ya wafungwa hao walitoroka, baada ya kituo cha polisi kushambuliwa Ijumaa iliyopita.