Akizungumza na waandishi wa habari kwa mara ya kwanza baada ya kutangazwa mshindi, rais mteule wa Kenya William Ruto alisisitiza kuwa sokomoko zilizoshuhudiwa kwenye ukumbi wa Bomas of Kenya wa kujumlisha kura hazitouondoa uhalali wa matokeo ya uchaguzi wa rais.
Kabla ya kumtangaza mshindi wa kinyanganyiro hicho, mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Kenya, IEBC, Wafula Chebukati, aliweka bayana kuwa makamishna wawili Boya Molu na Abdi Guliye pamoja na afisa mkuu mtendaji Hussein Marjan wanauguza majeraha.
Hayo yaliwasibu baada ya purukushani kuzuka Bomas of Kenya na kupelekea baadhi ya viongozi wanaoegemea upande wa Azimio la Umoja One Kenya kufukuzwa ukumbini.
Kwa upande mwengine, makamishna 4 wa tume ya IEBC wakiongozwa na naibu mwenyekiti Juliana Cherera, walijitenga na matokeo ya mshindi wa uchaguzi wa rais.
Ruto asema madai ya makamishna hayana mashiko huku upande wa Odinga ukiashiria mambo bado
Rais Mteule William Ruto hajazipa uzito kauli hizo na kusisitiza kuwa wajibu wa tume ya uchaguzi ni kumtangaza mshindi na mtazamo wa makamishna hauna mashiko.
Akiwa Bomas of Kenya, alipata fursa kukutana ana kwa ana na Profesa George Wajackoya wa chama cha Roots aliyewania urais na Waihiga Mwaure wa Agano aliyekubali kushindwa saa chache zilizopita na kutangaza kuwa anamuunga mkono rais mteule William Ruto.
Wakati huohuo, wasifu wa William Ruto kwenye mtandao wa Twitter umebadilishwa na kumtambua kuwa rais mteule.
Mgombea mwenza wa Azimio la Umoja One Kenya, Martha Karua, amedokeza kupitia mtandao wa Twitter kuwa huenda wakaelekea mahakamani kudai haki kufuatia matokeo ya uchaguzi wa rais yaliyowanyima ushindi.
Ifahamike kuwa ilikuwa mara ya tano na huenda ikawa ya mwisho kwa waziri mkuu wa zamani Raila Odinga - mwenye umri wa miaka 77- kuwania urais wa Kenya.
Vurugu zazuka maeneo yenye wafuasi wengine wa Odinga huku wafuasi wa Ruto wakiserebuka
Yote hayo yakiendelea,vurugu ziliripotiwa katika baadhi ya maeneo yanayoaminika kuwa ngome za Azimio la Umoja One Kenya.Mjini Kisumu, kuliripotiwa rabsha baada ya matokeo ya uchaguzi wa rais kuwanyima fursa ya kusherehekea.
Kwenye mitaa ya Kibera, Mathare, Kawangware, barabara ya Jogoo,Baba Dogo na mitaa miengine ya mabanda vurugu zilishuhudiwa.
Wakati huohuo, wakaazi wa miji ya eneo la Mlima Kenya wanaendelea na sherehe.
Mjini Karatina,ambako ndio makazi ya naibu wa rais mteule Rigathi Gachagua,wakaazi waliserebuka na kuimba walipomiminika barabarani.
Kwa sasa naibu wa rais mteule Rigathi Gachagua ametambuliwa kuwa sheha wao katika eneo la Mlima Kenya.
Biashara zilifungwa katika miji ya Kutus, Ngurubani, Kimunye na mengine wakati wakaazi walipomiminika majiani kusherehekea ushindi wa Kenya Kwanza.
Polisi yawasifu raia kwa kuonesha utulivu na kulinda amani
Licha ya matukio ya rapsha za hapa na pale, Inspekta mkuu wa polisi Hillary Mutyambai amewapongeza wakenya kwa kudumisha amani katika kipindi hiki cha uchaguzi.
Kwenye taarifa yake, inspekta mkuu wa polisi alielezea kuwa hali imekuwa shwari kiusalama tangu Agosti tarehe 9 .
Hatimaye, kesi za uchaguzi zitasikiliwa kwenye mahakama ya juu kwenye kitengo cha jumba la Forodha hapa jijini Nairobi.
Kwa mujibu wa taifa ya msajili wa mahakama ya juu L M Wachira, malalamishi rasmi yanapaswa kuwasilishwa mahakama kabla ya saa nane mchana ya siku iliyoteuliwa.