WILHELMSHAVEN: Vikosi vya wanamaji vinaelekea Lebanon
22 Septemba 2006Matangazo
Kikosi cha kwanza cha jeshi la wanamaji la Ujerumani kimeondoka bandari ya kaskazini ya Wilhelmshaven kuelekea Bahari ya Mediterania,siku moja baada ya wabunge kutoa idhini ya kushiriki katika ujumbe wa kulinda amani nchini Lebanon. Kiasi ya wanamaji 1,000 katika manowari nane wanatazamiwa kuwasili mwambao wa Lebanon katika muda wa siku 14.Waziri wa ulinzi wa Ujerumani, Franz Josef Jung alipozungumza katika sherehe ya kuadhimisha safari ya wanamaji hao alisema,ujumbe huo ni wa kihistoria.Ujerumani itapeleka hadi wanajeshi 2,400 kama sehemu ya vikosi vitakavyopiga doria katika mwambao wa Lebanon ili kuzuia usafirishaji wa silaha kwa wanamgambo wa Hezbollah.