Wikileaks
1 Desemba 2010Polisi ya kimataifa Interpol imemtaja Julian Assange mmiliki wa mtandao wa Wikileaks kuwa miongoni mwa watu wakuu inayowasaka. Waranti ya kukamtwa kwa Assange iliyotolewa na Interpol ina maana kwamba huenda Assange akakamatwa kokote. Hapo awali mmiliki huyo wa Wikileaks alikata rufaa dhidi ya amri ya kukamtwa kwake iliyotolewa na Sweden kwa kumtuhumu kwa ubakaji.
Mahakama ya mjini Stockholm ilitoa waranti ya kukamatwa Assange siku kumi zilizopita.Taarifa kuhusu aliko Assange hazijulikani.
Kwa upande wake Marekani inaonekana kufikiria kumshtaki mmiliki wa mtandao wa Wikileaks kwa makosa ya ujasusi baada ya mtandao huo kuchapisha nyaraka za siri za kidiplomasia kwa vyombo vya habari.
Huku hayo yakijiri, mtandao huo umesema umevamiwa na ulizimika kwa masaa katika nchi kadhaa hapo jana. Katika mahojiano na jarida la Forbes, Assange amesema anapanga kulilenga soko la hisa la Wallstreet Marekani mwaka ujao. Assange ambaye ni mzaliwa wa Australia, amesema amepanga kufanya ufichuzi mkubwa wa nyaraka zinazohusu taasisi moja kubwa ya kifedha Marekani, itakayofichua nyenendo haramu zitakazo sababisha kufungwa kwa benki moja au mbili.
Mwandishi: Maryam Abdalla/ Afp/Ap/Dpae