1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO yasema maambukizi ya corona yaongezeka tena Ulaya

2 Julai 2021

Shirika la afya duniani WHO limetoa wito wa kuweka njia bora zaidi katika kufuatilia mashindano ya kandanda ya kugombea kombe la Ulaya wakati ambapo maambukizi ya corona yanaongezeka tena barani Ulaya.

https://p.dw.com/p/3vuv6
EURO 2020 | Deutschland vs England
Picha: Justin Tallis/Getty Images/AFP

WHO imesema mamia ya watu wamegunduliwa kuwa na maambukizi hayo, miongoni mwa watazamaji wa kandanda barani Ulaya kote. Mkuregenzi wa shirika la afya duniani kanda ya Ulaya Hans Kluge ametahadharisha juu ya hatari ya kuzuka wimbi jipya la maambukizi ikiwa nidhamu haitazingatiwa. Amesema maambukizi yaliongozeka kwa asilimia 10 wiki iliyopita kutokana na watu kukusanyika pamoja kwa wingi, kutokana na safari na kulegeza hatua za kudhibiti maambukizi.

Kluge amesema kitisho hicho cha kuongezeka maambukizi kinatokana na kuwepo aina mpya ya virusi vya corona kwa jina Delta vinavyosambaa kwa kasi tangu kubainika kwa mara ya kwanza nchini India.

Mkurugenzi wa WHO kanda ya Ulaya Hans Kluge
Mkurugenzi wa WHO kanda ya Ulaya Hans KlugePicha: Alberto Pizzoli/AFP/Getty Images

Mkuregenzi wa shirika la afya duniani kanda ya Ulaya  Hans Kluge ameongeza kusema kuwa kutokana na idadi hiyo ya maambukizi, hakuna mahala ambako janga hilo limeondoka na kwamba yatakuwa makosa makubwa kwa raia na viongozi kufikiri kwamba janga hilo limetoweka. Amesema lengo lake sio kuwavurugia furaha mashabiki wa kandanda lakini anashauri kwamba kabla ya kusafiri kwenda kuwashangilia wachezaji wetu inatupasa sote tuwe waangalifu!

Mpaka sasa watu zaidi ya milioni 3.9 wameshakufa duniani kote kutokana na janga la corona. Mkurugenzi huyo wa shirika la afya duniani WHO kanda ya Ulaya Hans Kluge amesema inapasa kuwa na nidhamu la sivyo maambukizi yataongezeka zaidi.

Mchuano uliojaza mashabiki ni kati ya Ujerumani na Uingereza  uliochezwa kwenye uwanja wa Wembley jijini London tarehe 29 Juni 2021.
Mchuano uliojaza mashabiki ni kati ya Ujerumani na Uingereza uliochezwa kwenye uwanja wa Wembley jijini London tarehe 29 Juni 2021.Picha: Catherine Ivill/REUTERS

Katika juhudi za kulinda afya, shirikisho la vyama vya kandanda barani Ulaya, UEFA limebatilisha tiketi zote walizouziwa watu nchini Uingereza kwa ajili ya mechi ya robo fainali kati ya England na Ukraine itakayochezwa mjini Rome mwishoni mwa wiki hii.

Urusi nayo imetoa taarifa kwa mara ya tatu juu ya kuongezeka kwa idadi kubwa ya vifo kutokana na maambukizi ya virusi vya corona, wakati nchini Uingereza maambukizi yanaongezeka licha ya zoezi  kabambe la kutoa chanjo. Mechi za nusu fainali na fainali za kombe la Ulaya zitachezwa nchini Uingereza wiki ijayo.

Chanzo:/AFP