WHO yatafakari uteuzi wa Mugabe kama balozi wake
22 Oktoba 2017Mapema wiki hii, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni - WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus alikuwa amemuomba Robert Mugabe, kiongozi wa kiimla wa Zimbabwe mwenye umri wa miaka 93 kuwa Balozi wa Nia Njema, katika kupambana na magonjwa yasioambukiza kama vile maradhi ya moyo, kiharusi, pumu na kadhalika.
Uteuzi huo ulizichanganya nchi muhimu wanachama wa WHO na wanaharakati katika sekta ya afya, ambao wameeleza kuwa mfumo wa afya nchini Zimbabwe umesambaratika nchini Zimbabwe chini ya uongozi wa Rais Mugabe.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Twitter, Tedros ambaye awali alikuwa waziri wa afya wa Ethiopia amesema, ''Nasikiliza, na nasikia wasiwasi wenu. Natafakari hatua kulingana na maadili ya WHO. Nitatoa tangazo haraka iwezekanavyo''.
Amumwagia sifa Mugabe
Akitangaza uteuzi wa Rais Mugabe katika mji mkuu wa Uruguay, Tedros alikuwa ameisifu Zimbabwe, kama nchi ambayo sera yake ya afya kwa wote inahakikisha huduma ya afya kwa kila mwananchi.
Uingereza, Canada na Marekani, Jumamosi ziliungana na wale wanaopaza sauti kupinga uteuzi wa Robert Mugabe katika nafasi hiyo. Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilitoa tangazo ikisema, ''uteuzi huu unakiuka wazi wazi maadili ya Umoja wa Mataifa ya kuheshimu haki za binadamu na heshima kwa ubinadamu''.
Uingereze ilisema uamuzi wa kumteuwa Mugabe ulikuwa ''wa kushangaza na wa kuvunja moyo, kwa kutilia maanani vikwazo ambavyo amewekewa na Marekani na Umoja wa Ulaya hivi karibuni''.
Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau alisema aliposikia uteuzi huo aliutaja kuwa ''usiokubalika kabisa'', alidhani ni mzaha wa siku ya wajinga, Aprili mosi.
Ukosoaji kutoka ndani ya Zimbabwe
Mwanaharakati wa haki za binadamu raia wa Zimbabwe, Doug Coltalt, kupitia mtandao wake wa Twitter alidhihaki, ''Mtu anayesafiri kwa ndege kwenda kupata matibabu nchini Singapore, kwa sababu ameharibu mfumo wa afya wa Zimbabwe, ameteuliwa kuwa Balozi wa Nia Njema wa WHO''.
Robert Mugabe ambaye anaiongoza Zimbabwe tangu mwaka 1980, hufanya safari za mara kwa mara kwenda nje ya nchi, kupata matibabu huku afya yake ikizidi kudhoofika.
Ndani ya Zimbabwe, waziri wa fedha wa zamani Tendai Biti, alisema uamuzi wa WHO kumteuwa Mugabe kama balozi wake, umedhihirisha jinsi shirika hilo lisivyoelewa siasa za Zimbabwe. Biti alisema hospitali kuu ya nchi hiyo haina maji ya bomba, na kwamba kila mgonjwa anayelazwa anatakiwa kuja na maji yake mwenyewe.
Msemaji wa chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe, Movement for Democratic Change - MDC, Obert Gutu, amesema uteuzi kama huo wa WHO, utazifanya taasisi za Umoja wa Mataifa kupoteza heshima.
Mwandishi: Daniel Gakuba/dpae, afpe
Mhariri: John Juma