1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO yasema vifo vya watoto wachanga vyaongezeka Gaza

2 Aprili 2024

Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema vifo vya watoto wachanga vimeongezeka kwa kasi katika Ukanda wa Gaza, huku watoto wakizaliwa na uzito mdogo, wakati huu mashambulizi ya Israel yakiendelea kwenye Ukanda huo.

https://p.dw.com/p/4eME2
Hospitali ya Al-Shifa
Muhudumu wa afya akiwahudumia watoto wachanga waliozaliwa katika hospitali ya Al-Shifa kabla ya kuhamishwa kutokana na kushambuliwa na kubomolewa na wanajeshi wa Israel.Picha: Hatem Ali/AP Photo/picture alliance

Msemaji wa WHO, Margaret Harris, alisema siku ya Jumanne (Aprili 2) mjini Geneva, Uswisi, kwamba katika hospitali pekee ya watoto kaskazini mwa Gaza ya Kamal Adwan, angalau watoto 15 wenye utapiamlo hupokelewa kwa siku, na mahitaji yanazidi kuwa makubwa zaidi.

Akizungumzia kushambuliwa hospitali za Gaza, Harris alisema ni sawa na kuuangamiza kabisa mfumo wa huduma ya afya kwenye Ukanda huo.

Soma zaidi: WHO: Hospitali 20 kati ya 36 za Gaza hazifanyi kazi tena

"Kuharibu hospitali ya al-Shifa kunamaanisha kuuangamiza kabisa mfumo wa afya. Kilikuwa kituo kikubwa cha huduma muhimu. Ilikuwa hospitali kubwa yenye vitanda 750, vyumba 25 vya upasuaji, vyumba 30 vya wagonjwa mahututi. Yaani, ilikuwa mahali ambapo watu huelekea ili kupata huduma bora inayoweza kutolewa na mfumo wa afya, ambayo sote katika jamii zetu tunatarajia kuzipata tunapozihitaji." Alisema.

Soma zaidi: Blinken kuzungumza na Macron juu ya Ukraine, Gaza

Hata hivyo, shirika la WHO lilisema haliwezi kutoa takwimu sahihi za vifo vya watoto kutokana na uharibifu mkubwa katika eneo la Palestina baada ya miezi sita ya vita kati ya Israel na kundi la Hamas, huku akisisitiza kuwa watu wengi hawafiki hospitalini.

Hayo yakijiri, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amekiri kuwa nchi yake imehusika katika kile alichokiita shambulio la kusikitisha na ambalo halikukusudiwa dhidi ya wafanyakazi wa shirika la misaada la World Central Kitchen (WCK) huko Gaza.