WHO yaonya watu kutokuwa na hofu iliyopitiliza kuhusu Corona
18 Februari 2020Dunia inazidi kutikiswa na kusambaa kwa Virusi vya Corona ambavyo sasa vinatambulika kama virusi vya COVID-19 huku watu zaidi ya 70,500 wakiambukizwa virusi hivyo nchini China pekee na mamia ya wengine kuambukizwa katika sehemu nyengine duniani.
Kando na hofu ya kimatibabu, Janga hilo la Corona pia limeathiri maisha ya kawaida ya wengi huku watu wakilazimika kufuta safari za ndege, mechi za kimataifa kuahirishwa, mashindano ya mbio na hafla mbalimbali duniani kufutwa.
Nchini Japan, serikali imewatolea wito raia wake kuepuka mikusanyiko ya watu na pia imefuta hafla mbalimbali za umma ikiwemo maadhimisho ya kila mwaka yanayofanyika katikati mwa mji wa Tokyo kwa ajili ya kusherekea siku ya kuzaliwa kwa mfalme.
Na katika mji wa Beijing mamlaka imetoa agizo la kuwatenga na kuwachunguza watu wanaofika mjini humo kwa siku 14, muda ambao iwapo mtu ameambukizwa Virusi hivyo vitajitokeza waziwazi.
Virusi vya Corona huenda vikawa na athari kubwa kwa uchumi wa China
Maafisa wa China wanasema kuwa virusi vya Corona vitakuwa na athari kubwa kwa uchumi wa taifa hilo.
"Ndege hazifanyi tena kazi katika maeneo makubwa wakati wa sherehe za msimu wa machipuko, hilo limesababisha abiria wengi kurudisha tiketi zao. Kwanzia Januari 20 hadi Februari 13, mashirika matatu ya ndege yamerudisha tiketi milioni 13, wamefuta safari 78,000 za ndege na idadi ya abiria wanaotumia usafiri wa ndege inazidi kushuka kila siku," amesema Naibu mkurugenzi wa tume ya usimamizi wa Mali nchini humo Ren Hongbin.
Aidha chombo cha habari cha serikali kimesema kuwa huenda China ikahairisha vikao vyake vya bunge ambavyo vimekuwa vikifanyika kila mwezi wa Machi katika muda wa miaka 35.
Wakati hayo yanaendelea, serikali za Canada, Australia, Italia na Hong Kong ziko mbioni kuwaondoa raia wake kutoka meli ya Japan. Hii ni baada ya Marekani kutuma ndege kuondoa raia wake kwenye meli hiyo na kuwasafirisha hadi nchini mwao. Raia hao wa Marekani wamewekwa kwenye karantini kwa ajili ya kuchunguzwa.
Yamkini mlipuko wa Virusi hivyo vya Corona pia umewakosesha usingizi wadau wa afya baada ya Mkuu wa shirika la afya duniani Tedros Adhanom kukiri kuwa sio rahisi kutabiri mwelekeo gani virusi hivyo vitachukua.
Chanzo AFP/Reuters