WHO yaanza kutoa chanjo ya Ebola huko DRC
8 Agosti 2018Shirika la afya duniani WHO limesema wataalamu wake wanaanza kutoa chanjo ya Ebola nchini Congo, kufuatia mripuko mbaya wa karibuni wa ugonjwa huo.
Maafisa wa afya wameonya juu ya ugumu wa kudhibiti ugonjwa huo kutokana na uwepo wa makundi mbalimbali ya uasi katika jimbo la kaskazini-mashariki mwa nchi hiyo, linalopakana na Uganda na Rwanda.
Wizara ya afya ya Congo inasema watu wasiopungua tisa wamefariki katika mripuko huo wa kumi wa Ebola nchini humo, uliotangazwa Agosti 1.
Kumekuwepo na visa 16 vilivyothibitishwa, visa 27 vinavyofikiriwa kuwa ni Ebola, na watu 46 wanaoshukiwa kuwa na virusi hivyo.
Chanjo hiyo ya majaribio ilitumiwa katika mripuko wa awali usiohusiana na wa sasa, uliotangazwa kumalizika mwezi uliopita. Watu wa kwanza kupatiwa chanjo hiyo ni wafanyakazi wa afya, watu waliogusana na wagonjwa waliothibitika kuwa na Ebola na wale waliowasiliana nao.