1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO: Maambukizi ya COVID-19 yanaongezeka duniani

19 Julai 2020

Shirika la Afya Duniani WHO limeripoti kwa siku ya pili mfululizo juu ya kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya corona duniani, huku jumla ya visa vya vipya ikipindukia 259,000 katika muda wa saa 24 zilizopita.

https://p.dw.com/p/3fXpk
Äthiopien Addis Ababa | Medizinisches Personal
Picha: Getty Images/AFP/A. Sileshi

Kwa mujibu wa taarifa ya kila siku ya WHO maambukizi makubwa kwa siku ya Jumamosi yamerikodiwa nchini Marekani, Brazil, India na Afrika ya Kusini.

Takwimu za siku ya Ijumaa zilionesha kulikuwa na visa vipya 237,000 huku idadi ya watu wanaokufa kwa siku kutokana na ugonjwa wa COVID-19 imepanda katika siku za karibuni ikilinganishwa na miezi wiki chache zilizopita.

Kulingana na tarakimu zilizojumuishwa na shirika la habari la Reuters visa vya virusi vya corona duniani vilipindukia milioni 14 siku ya Ijumaa na janga hilo tayari limewauwa karibu watu 600,000 katika kipindi cha miezi saba iliyopita.

Wimbi hilo la maambukizi linaashiria visa milioni vimerikodiwa chini ya saa 100 zilizopita.

Maambukizi yachachamaa Afrika Kusini 

Südafrika Johannesburg Soweto | Verbot von Alkohol
Eneo la Soweto nchini Afrika Kusini Picha: picture-alliance/AP Photo/T. Hadebe

Afrika Kusini imekuwa moja ya mataifa matano yaliyoathiriwa zaidi na janga la virusi vya corona, katika wakati ambapo maambukizi mapya kote duniani yanaashiria maisha ya kawaida hayatorejea hivi karibuni.

Idadi ya visa vya maambukizi 350,879 vilivyothibitishwa nchini Afrika Kusini ni karibu nusu ya visa vyote vilivyorikodia barani Afrika na juhudi zake za kukabiliana na janga hilo ni ishara ya matatizo yatakayowakumba mataifa yaliyo na mifumo dhaifu ya afya barani humo.

Afrika Kusini sasa iko nyuma ya Marekani, Brazil, India na Urusi kwa idadi ya maambukizi.

"Ukweli ni kwamba raia wengi wa Afrika Kusini ni kama bata waliopumzika kwa sababu hawawezi kutii miongozo ya WHO ya kuboresha hali ya usafi na kujitenga " amesema Askofu Mkuu wa Afrika Kusini na mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel Desmond Tutu katika taarifa iliyotolewa kwa pamoja na mkewe.

Mataifa mengine hali inatishia mashaka 

Nchini Marekani, vikosi vya matabibu wa kijeshi vimepelekwa mjini Texas na California kuzisaidia hospitali zilizozidiwa na idadi kubwa ya wagonjwa.

Indien Kalkutta | Coronavirus | Protest gegen Distanz-Regeln
Raia wa India wakitekeleza sharti la kujitengaPicha: DW/P. Samanta

Wimbi la mamabukizi linamaanisha mamilioni ya watoto nchini Marekani hawatoweza kurejea shuleni kikamilifu wakati wa majira ya mapukutiko.

Huko India, wimbi la visa vipya 34,884 vimeripotiwa ndani ya siku moja huku seirkali za mitaa zikiendelea kurejesha vizuizi katika maeneo mahsusi ya taifa hilo lenye zaidi ya wakaazi bilioni 1.

Nchini Iran, rais wa taifa hilo ametoa tangazo la kushtua kwamba huenda raia milioni 25 wameambukiwa virusi vya corona.

Rais Hassan Rouhani amekariri utafiti mpya wa wizara ya afya ambao bado haujachapishwa hadharani.

Iran ndiyo taifa lililoathiriwa vibaya na janga la virusi vya corona katika eneo la mashariki ya kati ikiwa na visa 270,000 vilivyothibitishwa.

Mwandishi: Rashid Chilumba

Mhariri: Bruce Amani