1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO kuzifanyia utafiti dawa za mitishamba juu ya COVID-19

22 Julai 2020

Shirika  la  afya  ulimwenguni WHO na  kituo cha udhibiti wa  magonjwa  barani Afrika CDC yameanzisha juhudi kuangalia uwezekano wa madawa ya mitishamba katika kupambana  na  janga  la  virusi vya  corona.

https://p.dw.com/p/3fhb7
Afghanistan Coronavirus und traditionelle Medizin
Picha: DW/S. Tanha

Jopo hilo  jipya la ushauri litaunga mkono nchi katika majaribio ya kitabibu, utafiti mwingine na utengenezaji wa dawa nyingine za  kienyeji  wakati hivi  sasa  janga likisambaa kwa  kasi  katika  baadhi  ya sehemu  za  bara la  Afrika. Kesi zilizothibitishwa  katika  bara  hilo zimekaribia  kufika  750,000, zaidi  ya  nusu zikiorodheshwa  nchini  Afrika  kusini.

Taarifa  ya  WHO imesema  dawa  za  asili, zina  faida nyingi na  bara  hilo lina  historia  ndefu  ya  matumizi yake. Mkuu  wa  WHO  barani  Afrika Matshidiso Moeti amesema  utafiti unapaswa  kuwekwa katika  misingi  ya kisayansi.

Mataifa  kadhaa  yalionesha  shauku  baada  ya  rais  wa Madagascar kutangaza  dawa  ya  mitishamba  kama sehemu ya  taifa  hilo  la  kisiwani  kupambana  na  janga la  virusi  vya  corona.

Guinea-Bissau Coronavirus Tee aus Madagaskar
Dawa ya mitishamba ya Madagascar inayodaiwa kuponya kirusi cha coronaPicha: DW/B. Darame

Maambukizi duniani

Maambukizi  ya  virusi  vya  corona  duniani  yameongezeka kupindukia  watu  milioni  15 kufikia siku ya Jumatano, kwa  mujibu wa idadi  iliyowekwa pamoja na  shirika  la  habari  la  Reuters, wakati  ugonjwa  huo ukishika  kasi  hata wakati  nchi bado  zinaendelea kutofautiana  katika  jibu  lao  dhidi  ya  janga  hilo. 

Nchini  Marekani, nchi  ambayo  ina idadi  kubwa ya maambukizi duniani ikiwa  na  watu milioni 3.91 ya walioambukizwa, rais Donald Trump alionya, kuwa huenda hali  itakuwa  mbaya  zaidi  kabla  ya  kutengemaa. 

Nchi  tano  za  juu ambazo  zina  maambukizi  makubwa  ni  pamoja  na  Brazil, India, Urusi na  Afrika  kusini. Lakini idadi iliyowekwa pamoja na shirika  la  habari  la Reuters inaonesha  ugonjwa huo unasambaa  kwa  kasi  katika  mataifa  ya  Amerika, ambayo yana zaidi  ya  nusu ya maambukizi  duniani  kote na  nusu  ya  vifo. Duniani kote pia kiwango cha  maambukizi hakioneshi  ishara ya kupungua kasi.