1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiChina

WFP : Mabilioni yanahitajika kuepuka migogoro na njaa

1 Aprili 2023

Mkuu wa WFP David Beasley, ameonya kuwa bila mabilioni ya dola zaidi ya kulisha mamilioni ya watu wenye njaa, ulimwengu utashuhudia migogoro mbali mbali katika muda wa miezi 12 hadi 18 ijayo.

https://p.dw.com/p/4PZzy
Äthiopien Bewohner des Kriegsgebiets in der Nord Wollo Zone haben Angst vor einer Hungersnot
Picha: Alemenew Mekonnen/DW

Katika mahojiano kabla ya kukabidhi uongozi wa shirika hilo kubwa zaidi la kiutu duniani kwa balozi wa Marekani Cindy MacCain wiki ijayo, Beasley amesema ana wasiwasi mkubwa kwamba WFP haitaweza kufikisha dola bilioni 23 zinazohitajika mwaka huu kuwasaidia takriban watu milioni 350 katika mataifa 49 wanaohitaji sana chakula. Beasley ameongeza kuwa WFP iko katika mzozo sawa na mwaka jana lakini kwa bahati nzuri, ameweza kuishawishi Marekani kuongeza msaada wake kutoka dola bilioni 3.5 hadi 7.4 na Ujerumani kutoka dola milioni 350 hadi dola bilioni 1.7 miaka michache iliyopita lakini hafikirii zitafanya tena hivyo mwaka huu.

Mataifa mengine yanapaswa kuongeza msaada

Beasley amesema kuwa mataifa mengine yanapaswa kuongeza misaada yao kuanzia na China ambayo ni taifa la pili kubwa kwa uchumi duniani ambalo lilitoa dola milioni 11 pekee kwa WFP mwaka jana. Beasley aliipongeza China kwa mafanikio yake katika kupunguza kwa kiasi kikubwa njaa nchini humo, lakini akasema imetoa chini ya senti moja kwa kila mtu mwaka jana ikilinganishwa na Marekani inayoongoza kiuchumi duniani ambayo ilitoa dola 22 kwa kila mtu.

Mataifa ya Ghuba yanaweza kutoa msaada zaidi

Hungerkatastrophe in Afrika
Mkimbizi wa Somalia apokea msaada wa ngano kutoka WFP katika kambi DadaabPicha: picture alliance/dpa

Mkuu huyo wa WFP amesema kwa kuweko kwa bei za juu za mafuta, mataifa ya ghuba yanaweza kutoa msaada zaidi hasa mataifa ya kiislamu ambayo yana uhusiano na mataifa katika eneo la Afrika Mashariki, eneo jangwa la Sahara na kwengineko katika Mashariki ya Kati, huku akielezea matumaini kwamba mataifa hayo yataongeza kiwango chao cha msaada.

Beasley amesema mabilionea tajiri zaidi walipata faida ambayo haijawahi kutokea wakati wa janga la COVID-19, na kwamba sio jambo kubwa kuwaomba baadhi ya matajiri hao kujitokeza kusaidia katika mgogoro huo wa muda mfupi ijapokuwa misaada sio suluhisho la muda mrefu la mgogoro wa chakula.

Viongozi ya Magharibi na Ulaya hawapaswi kuangazia Ukraine na Urusi peke yake

Beasley ameongeza kuwa viongozi wa Magharibi na Ulaya wanapoangazia zaidi Ukraine na Urusi, hawapaswi kusahau maeneo yao ya Kusini na Kusini Mashariki kwasababu yasiposhughulikiwa yatawaathiri. Kiongozi huyo amesema viongozi hao wanapaswa kutoa kipaombele kwa mahitaji ya kibinadamu ambayo yatakuwa na athari kubwa kwa uthabiti wa jamii duniani. Alitaja maeneo kadhaa ya kipaombele ambayo ni eneo la Sahel barani Afrika pamoja na eneo la Mashariki linalozijumuisha Somalia, Kaskazini mwa Kenya, Sudan Kusini na Ethiopia, pamoja na Syria inayoziathiri Jordan na Lebanon.