1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Westgate yafungua mlango kwa Kenyatta

Admin.WagnerD26 Septemba 2013

Wakati shambulio dhidi ya kituo cha Westagate mjini Nairobi linaathiri sekta ya utalii na uwekezaji nchini Kenya, wachambuzi wanasema pia linatoa fursa kwa rais wa nchi hiyo kujinasua katika mtego wa mahakama ya ICC.

https://p.dw.com/p/19p6d
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta akizungumzia shambulizi la kigaidi dhidi ya kituo cha biashara cha Westgate mjini Nairobi.
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta akizungumzia shambulizi la kigaidi dhidi ya kituo cha biashara cha Westgate mjini Nairobi.Picha: John Muchucha/AFP/Getty Images

Washirika wa rais Kenyatta wanatoa hoja kwamba athari za shambulio la Jumamosi iliyopita kwa usalama wa Afrika na dunia nzima ndiyo unapaswa kupewa kipaumbele kuliko kuliko wajibu wa rais huyo kwa mahakama ya ICC, ambako anatakiwa kujibu mashtaka Novemba 12.

Akituhumiwa na waendesha mashtaka katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu kwa kuandaa machafuko ya baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007/2008, Kenyatta anaongoza taifa ambalo linatizamwa kama mhanga wa uhalifu unaoweza kuadhibiwa chini ya sheria ya kimataifa.

Kituo cha biashara cha Westgate Mall kilichoshambuliwa na wapiganaji wa Al-Shabaab. ***FREI FÜR SOCIAL MEDIA***
Kituo cha biashara cha Westgate Mall kilichoshambuliwa na wapiganaji wa Al-Shabaab.Picha: Reuters

Shambulio la Jumamosi dhidi ya kituo cha Westgate, ambalo kundi la waasi la Al-Shabaab limedai kuhusika nalo, limeipatia Kenya maneno ya uugwaji mkono na kulaani ugaidi kutoka kwa viongozi mbalimbali duniani.

Usalama muhimu kuliko ICC
Hii inaweza kuhamisha mandhari ya kidiplomasia kwa rais huyo mwenye umri wa miaka 51, ambaye kuchaguliwa kwake mwezi Machi kuiongoza Kenya kuliongeza mwelekeo mpya katika mashtaka ya ICC dhidi yake.

Moses Kuria, mpanga mikakati katika muungano wa Kenyatta wa Jubili, anasema siyo busara kutoa kipaumbele kwa ICC wakati yapo mambo mengi yanayopaswa kufanywa nchini Kenya kwa wakati huu, na anapendekeza kuwa ICC isitishe mashtaka dhidi ya Kenyatta na naibu wake William Ruto, kwa angalau miaka miwili au mitatu, ili kuwapa nafasi kukabiliana na kitisho cha usalama, ambacho rais huyo wa Kenya amekiita "vita vya kimataifa."

Majaji wa ICC siku ya Jumatatu waliahirisha kesi ya Ruto kwa wiki moja ili kumuwezesha kurudi nyumbani kushughulikia mgogoro wa shambulizi dhidi ya kituo cha Westgate. Msemaji wa ICC Fadi El-Abdallah alisema mawakili wa Kenyatta waliwasilisha ombi la kutaka rais huyo asifike mwenyewe mjini The Hague kwa ajili ya kesi yake, bali ashiriki kwa njia ya vidio.

Makamu wa rais wa Kenya William Ruto.
Makamu wa rais wa Kenya William Ruto.Picha: Reuters

Nchi za magharibi kulegeza msimamo wao?
Serikali za mataifa ya magharibi, ambazo zinalaazimika kuchukua tahadhari katika namna zinavyohusiana na washtakiwa hao wa ICC baada ya kuchaguliwa kwao, sasa zinaonekana kuwa tayari kushirikiana nao kwa karibu, hasa katika masuala ya kupambana na ugaidi. Mkurugenzi wa Afrika katika Umoja wa Ulaya, Nick Westcott, ambaye alikuwa mjini Nairobi kujadiliana na serikali juu ya athari za shambulio la Jumamosi, alisema anachukulia haja ya kupambana na ugaidi kuwa suala muhimu.

Alipoulizwa iwapo hili litamaanisha kulegeza msimamo zaidi kwa mataifa ya magharibi katika uhusiano wake na Kenyatta, Westcott alisema masuala mawili - ambayo ni kesi ya kiongozi huyo wa Kenya katika ICC na jukumu lake la kimataifa katika mapambano dhidi ya itakadi kali za dini vinapaswa kutenganishwa. Lakini aliongeza kuwa ni muhimu kuwa wanashirikiana kwa karibu kadri iwezekanvyo, kushghulikia vitisho kama kile cha Kenya, nchini Somali na kwingineko.

Akiaksi ushirikiano ulioongezeka, waziri wa mambo ya ndani wa Kenya Joseph ole Lanku, alisema Marekani, Israel, Uingereza, Ujerumani, Canada na polisi ya kimataifa Interpol, walikuwa wakisaidia katika uchunguzi wa tukio la Westagate, na utambuzi wa washambuliaji.

Makao makuu ya mahakama ya ICC mjini The Hague.
Makao makuu ya mahakama ya ICC mjini The Hague.Picha: Getty Images

Wengine wataka haki itendeke
Lakini kwa wale wanaotaka Kenyatta akabiliwe na mkono wa sheria, na kukomesha utamaduni wa uhuru wa kutoadhibiwa barani Afrika, wanasisitiza kuwa laazima kesi ya ICC iendelee, kwa hoja kwamba ingawa tukio la Westgate lilikuwa la kutisha, idadi ya watu waliouawa katika tukio hilo, ni sehemu tu ya wale waliouawa katika machafuko ambayo Kenyatta anashtakiwa kwa kuyapanga.

Shirika la ushauri kuhusu hatari za kimataifa la Maplecroft, lilisema shambulio la Al-Shabaab lilionyesha jinsi mashtaka ya ICC yanavyoweza kuvuruga shughuli za kiutawala nchini Kenya, na lilisema katika taarifa kuwa shambulio hilo linatoa fursa kwa Kenyatta na Ruto kudai kesi yao ihamishwe kutoka mjini The Hague, na kusikilizwa mjini Arusha Tanzania, au iahirishwe kwa ujumla.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman