1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wenye msimamo mkali wa dini ya kiislamu waandamana Sudan

5 Desemba 2022

Waandamana kupinga Umoja wa Mataifa kuingilia masuala ya ndani ya Sudan pamoja na makubaliano yaliyofikiwa kati ya viongozi wa kijeshi na muungano wa kiraia kuondowa mkwamo wa kisiasa

https://p.dw.com/p/4KToY
Sudan United Nations Demonstration
Picha: Mahmoud Hjaj/AA/picture alliance

Nchini Sudan maelfu ya wasudan  wenye msimamo mkali wa dini ya kiislamu mwishoni mwa juma waliandamana kupinga juhudi za Umoja wa Mataifa za kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa uliotokana na mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika mwaka jana.

Maandamano hayo yamekuja siku moja baada ya viongozi wa kijeshi na muungano wa vyama vya kiraia wenye sauti kutangaza mpango wa kufikia makubaliano ya awali. Saumu Mwasimba anayatazama maandamano hayo na kilichojitokeza huko Khartoum.

Proteste im Sudan
Picha: Marwan Ali/AP Photo/picture alliance

Maandamano hayo yalifanyika siku ya Jumamosi na yaliandaliwa na makundi ya kiisalamu yenye msimamo mkali na maelfu ya watu walijitokeza.

Maandamano hayo ndiyo ya hivi karibuni kabisa kuwahi kufanywa na makundi hayo na yamefanyika siku moja baada ya kutangazwa mipango ya kusainiwa makubaliano ya awali baina ya majenerali wa kijeshi na muungano wa kiraia.Maafisa wa Umoja wa Mataifa ni miongoni mwa walioshiriki kwenye mazungumzo kati ya viongozi hao wa kijeshi na muungano wa FFC mnamo siku ya Ijumaa.

Waandamanaji wanaopinga mpango wa kutiwa saini makubaliano ya awali wamesikika nje ya ofisi za Umoja wa Mataifa mjini Khartoum wakisema hawataki masuala ya ndani ya nchi yao yaingiliwe na Umoja huo.

Sudan Volker Perthes UN
Volker Perthes-Mwakilishi wa UN SudanPicha: ASSOCIATED PRESS/picture alliance

Baadhi wamesikika wakimtaka mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini humo Volker Perthes kuondoka Sudan.Miongoni mwa waandamaji ni Ahmed Omar anasema.

" Kusainiwa makubaliano na na kundi lisilofungamana na dini, FFC, hakuwakilishi watu wa Sudan na hatukubali kwasababu hatuungi mkono mitizamo ya kutofungamana na dini na hatutaki pendekezo lisilokuwa na mafungamano na dini.Sisi ni waislamu na tunataka katiba yetu  itokane na kitabu cha Quran na mfundisho ya mtume.''

Mkwamo wa kisiasa unaiandama Sudan tangu mkuu wa majeshi AbdelFatah al Burhan kuongoza mapinduzi ya kijeshi Oktoba mwaka jana,hatua iliyoukwamisha mchakato tete wa mpito wa kukabidhi majukumu kwa utawala wa kiraia,uliowekwa madarakani baada ya kuondolewa kwa nguvu uongozini mwaka 2019 aliyekuwa mtawala wa kiimla wa muda mrefu Omar Al Bashir.

Yamekuwa yakishuhudiwa  kiasi kila wiki maandamano ya kupinga mapinduzi,pamoja na mgogoro wa kiuchumi  wakati mapigano ya kikabila katika maeneo ya vijijini nchini humo yakiongezeka.

Mnamo siku ya ijumaa viongozi wa kijeshi walikutana na muungano mkubwa wa kiraia FFC ulioondolewa kwa nguvu madarakani na jeshi mwaka jana.FFC ukatoa tamko kuhusu majadiliano hayo na kwamba kimefikiwa kile kinachoweza kuwa makubaliano ya kisiasa ya awali ambayo huenda yakaweka msingi wa kuundwa utawala wa mpito wa kiraia.

Abdel-Fattah Burhan
Picha: Marwan Ali/AP/picture alliance

Baraza kuu la kijeshi la uongozi linaloongozwa la jenerali al Burhani likathibitisha kuhusu mpango huo.Walioshuhudia mazungumzo hayo ni maafisa kutoka Umoja wa Afrika,Umoja wa Mataifa na shirika la ushirikiano wa maendeleo wa kiserikali wa nchi za mashariki mwa Afrika IGAD.

Mwanasiasa mpinga rushwa aachiwa huru

Kwa upande mwingine mwanasiasa maarufu  Wagdi Salih mwanachama wa muungano wa FFC aliachiwa huru jana jumapili siku moja kabla muungano huo na viongozi wa kijeshi haujatia saini makubaliano ya awali ya kumaliza mkwamo wa kisiasa.

Ni kiongozi wa kisiasa aliyekuwa mstari wa mbele kuhakikisha imeundwa kamati ya kupambana na rushwa baada ya kupinduliwa utawala wa Omar al Bashir na kamati hiyo ilipewa jukumu la kuuvunja mtandao wa utawala wa Bashir.Lakini kamati hiyo ilikabiliwa na shinikizo kubwa kutoka kwa majenerali waliokuwa wakigawana madaraka na muungano wa kiraia FFC.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW