1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Weinstein alitaka kulala na Lupita Nyong'o

20 Oktoba 2017

Mwigizaji huyo mashuhuri kutoka Kenya anaeleza jinsi ambavyo Harvey Weinstein, meneja ya kampuni ya utengenezaji filamu, alimnyanyasa kijinsia. Weinstein anasakatwa na sakata la unyanyasaji wa wanawake kadhaa.

https://p.dw.com/p/2mGTs
Lupita Nyong’o
Picha: Getty Images/D. Dipasupil

Lupita ameliambia gazeti la New York Times kuwa alikutana na Harvey Weinstein kwa mara ya kwanza Berlin, Ujerumani, katika sherehe ya tuzo za filamu mwaka 2011. Kipindi hicho Lupita akiwa bado mwanafunzi katika chuo cha uigizaji nchini Marekani. Alikuwa na ndoto ya kuwa muigizaji mashuhuri duniani hivyo alipotambuliswa kwa Weinstein alifurahi. Lakini mwanamke mmoja ambaye naye alikuwa mtaalamu wa filamu alimuonya Lupita kwamba Weinstein ni mtu mzuri lakini wakati mwingine anaweza kuwa mwenye mabavu. Lupita alimpa Weinstein mawasiliano yake, akitumaini kwamba atashirikishwa kwenye kazi za mtayarishaji huyo.

Muda mfupi baada ya kukutana Berlin Weinstein alimualika Lupita nyumbani kwake Connecticut, Marekani, kuangalia filamu. Dereva aliyeagizwa kumchukua Lupita kutoka nyumbani kwake alimtaarifu kuwa wanaelekea katika mgahawa ambapo Weinstein alikuwa akimsubiri kwa chakula cha mchana kabla hawajaelekea nyumbani kwake. Wakiwa hapo Lupita aliagiza kinywaji kisicho na kilevi, jambo ambalo halikumfurahisha Weinstein. Baada ya mzozano Weinstein alimwambia mhudumu amletee Lupita kinywaji chenye kilevi kwani yeye ndiye anayelipia. Lupita hakupendezwa na hilo hivyo akaamua kunywa maji yaliyokuwa mezani. Walipofika nyumbani kwake Lupita na watoto wa Weinstein walikaa na kuanza kuangalia filamu. Baada ya dakika kumi na tano Weinstein alimuita Lupita akisema angependa kumuonyesha kitu. Lupita alikataa kwani alitaka kufanya kile alichoalikwa kufanya lakini alipoona Weinstein anamshinikiza sana alikubali ili kutobishana mbele ya watoto wa Weinstein. 

Wanawake wasema walibakwa na Weinstein

Weinstein ni mtengeneza filamu mwenye mafanikio na ushawishi mkubwa
Weinstein ni mtengeneza filamu mwenye mafanikio na ushawishi mkubwa Picha: Getty Images/AFP/Y. Coatsaliou

Weinstein alimpeleka chumbani kwake na kumwambia kuwa anataka kumkandakanda. Lupita alidhani Weinstein anatania lakini baada ya kuona kuwa Weinstein anamaanisha anachosema ilimbidi kuwaza kwa haraka jinsi ambavyo ataweza kujitoa katika sehemu hiyo tata. Akikumbuka alivyojifunza shuleni jinsi ya kumkanda mtu, Lupita alimshawishi Weinstein amruhusu amkande. Baada Lupitaya kumkanda mgongo, Weinstein alisema kwamba anataka kuvua suruali yake. Lupita alipatwa na hofu na kumwambia Weinstein kwamba hatafurahishwa na jambo hilo lakini Weinstein aliinuka na kuanza kuvua suruali yake. Hapo ndipo Lupita alipopata mwanya wa kutoroka na kusimama mlangoni. Lupita alimwambia Weinstein kama hawaendelei kuangalia filamu ile ni bora arudi zake shule. Pamoja na hayo, Lupita anasema upo wakati mwingine ambapo Weinstein alimwambia anataka kulala naye. Alipokataa, Weinstein alimtishia kwamba jambo hilo litakuwa na athari kwa kazi yake kama mwigizaji.

Lupita si mwanamke wa kwanza kudai kwamba Weinstein alimnyanyasa kijinsia. Katika wiki zilizopita, wanawake kadhaa, wakiwemo nyota wa Hollyowood kama vile Gwyneth Paltrow wamejitokeza kusema kwamba Harvey Weinstein aliwanyanyasa kijinsia, alijaribu kuwabaka ama aliwabaka. Weinstein ni mmiliki wa kampuni ya filamu inayofanya vizuri sana nchini Marekani. Kampuni ya Weinstein imetengeneza filamu maarufu kama Django Unchained, The Fighter na Mandela:  Long Walk to Freedom.

Mwandishi: Ruth Fredrick/ap

Mhariri: Elizabeth Shoo