1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa zamani auwawa Lebanon

28 Desemba 2013

Waziri wa zamani wa Lebanon, Mohamad Chatah, ambae alikuwa akipinga serikali ya rais Bashar al-Assad, ameuwawa kwa bomu Ijumaa (27.12.2013) tukio ambalo washirika wake wanalituhumu kundi la Hezbollah.

https://p.dw.com/p/1AhoM
Libanon Explosion in Beirut 27.12.2013
mripuko uliotekea Beirut 27.12.2013Picha: Reuters

Waziri wa zamani wa Lebanon, Mohamad Chatah, ambae alikuwa akipinga serikali ya rais Bashar al-Assad, ameuwaka kwa bomu(27.12.2013) washirika wake wanalituhumu kundi la Hezbollah.

Shambulio hilo lililotokea mjini Beirut ambalo vilevile limesababisha vifo vya watu wengine watano, linaifanya Lebanon, taifa jirani la Syria kutumbukia kwenye vurugu zaidi kufuatia mfululizo wa miripuko iliyotokana na migogoro ya kimadhehebu kati Washia na Wasunni katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Kundi la Hezbollah latuhumiwa

Waziri Mkuu wa Zamani Saad al-Hariri amelituhumu kundi la Hezbollah, kwa kifo cha Chatah, mwanasiasa mwenye umri wa miaka 62, kwa kusema " ni ujumbe mpya katika ugaidi". Kundi ambalo pia analihusisha na mauaji ya baba yake Rafik Hariri 2005.

Libanon Hisbollah Kämpfer
Wapiganaji wa kundi la HezbollaPicha: picture-alliance/AP Photo

Mripuko uliteketeza kabisa gari aliyokuwemo Chatah na kusababisha watu wengine 71 waliokuwa karibu na eneo hilo kujeruhiwa. Tukio hilo halikutokea mbali na mahala ambapo aliuwawa kiongozi aliekuwa na ushawishi mkubwa Muislamu wa madhehebu ya Sunni Waziri Mkuu wa Zamani, Rafik Hariri.

Hata hivyo kundi la Hezbollah ambalo limetuma wapiganaji wake kusaidia upande wa rais Assad dhidi ya waasi limelaana tukio hilo la mauaji ya Chatah.

Kuwania madaraka Lebanon

Mauaji ya Chatah yanaunganishwa na sababu za kuwania madaraka tangu mauwaji ya Hariri. Kitendo hicho kinafuatiwa na mfululizo wa mashambulio yalisababisha vifo vya wanasiasa wanaoipinga Syria, maafisa wa serikali na waandishi habari.

Rafiq Hariri Plakat Libanon
Waziri Mkuu wa zamani wa Lebanon rafiki HaririPicha: picture-alliance/dpa

Oktoba mwaka uliopita Jenerali Wissam al-Hassan mkuu wa usalama anaehusishwa na Hariri aliuwawa kwa mripuko wa bomu lililokuwa katika gari mjini Beirut. Chatah aliyekuwa mkoasaji wa kundi la Hezbollah, alikuwa kama mtu mwenye msukumo mkubwa katika harakati zijazo pembezoni mwa Saad al Hariri na mtu mwenye kupendwa na mataifa ya Magharibi.

Jumuiya ya kimataifa yalaani mauwaji

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry amesema mauwaji hayo ni hasara kubwa kwa Lebanon, watu wa Lebanon na Marekani kwa ujumla. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki moon amelaani mauwaji hayo jambo ambalo limetekelezwa na mataifa 15 yenye uanachama wa kudumu katika baraza la usalama la umoja wa mataifa.

Catherine Ashton Belgien Brüssel
Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya Catherine AshtonPicha: picture-alliance/dpa

Nae mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton ameonesha kusikitishwa kwake na kuwataka viongozi wa Lebanon kuungana pamoja kurejesha hali ya usalama katika taifa hilo. Akizungumzia tukio la mripuko huo , mkuu huyo wa sera za mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya amesema ongezeko la vurugu nchini Lebanon ni kitisho kikubwa.

Aidha ametoa wito wa kuundwa serikali mpya yenye uwezo wa kukabiliana na changamoto zinazolikabili taifa hilo. Ameongeza kusema Umoja Ulaya upo pamoja na watu wa Lebanon katika kuthibitisha ahadi yake ya umoja, uhuru, utulivu, mamlaka na mshikamano wa kitaifa wa Lebanon.

Mwandishi: Sudi Mnette RTR/AFP
Mhariri: Sekione Kitojo