1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa zamani ajitoa chama cha SPD

P.Martin26 Novemba 2008

Kujitoa kwa waziri wa zamani wa uchumi wa Ujerumani Wolfgang Clement kutoka chama cha Social Demokratik SPD baada ya kuwa mwanachama kwa miaka 38 ni mada kuu katika magazeti ya Ujerumani leo Jumatano.

https://p.dw.com/p/G2Js

Basi hebu tuanze moja kwa moja na mada hiyo.Gazeti la FLENSBURGER TAGEBLATT linasema:

Mwisho wa chama cha SPD haudhihirishwi na matokeo ya uchunguzi wa maoni ya umma,bali ni ile hali inayokutikana ndani ya chama chenyewe. Kujitoa chamani na lawama alizozitoa waziri huyo wa zamani,zimefichua jinsi maoni yao yanavyotofautiana.Kwa hivyo Clement amesema,anataka kupigania yale anayoamini na hawezi kufanya hivyo akibakia chamani.

Lakini gazeti la OFFENBACH-POST linahisi kuwa Clement hakujitoa chamani kwa sababu ya tofauti za maoni tu,bali ametanguliza zaidi nafsi yake kuliko maslahi ya chama.Na likiendelea linasema:

Badala ya kugombea mkondo mwingine wa kufuatw,ameamua kujitoa kabisa chamani.Hiyo inasikitisha,kwani amewavunja nguvu hata wale waliokuwa na msimamo mmoja kama yeye ndani ya chama.

Gazeti la WESTDEUTSCHE ZEITUNG kutoka Düsseldorf likiendelea na mada hiyo hiyo linauliza:

Je,chama cha SPD bado kinataka kufuata sera za ajira zinazonufaisha viwanda? Kweli kitakuwa na nguvu na imani ya kujiweka mbali na chama cha mrengo wa shoto Die Linke badala ya kupoteza uaminifu wake na kutupia jicho uwezekano wa kuunda serikali ya mseto kwa kushirikiana na Die Linke na chama cha Kijani?Kufuatia kashfa ya kushindwa kunda serikali katika mkoa wa Hessen na sasa Clement kujitoa chamani, kumebainisha waziwazi kuwa mkakati wa viongozi wawili wapya wa SPD yaani Münterfering na Steinmeier haukufanikiwa kutuliza mivutano iliyozuka ndani ya chama kuhusu mwongozo wake.

Sasa hebu tugeukie mada nyingine inayoendelea kugonga vichwa vya habari si huku Ujerumani tu bali kote duniani-yaani msukosuko wa uchumi na taasisi za fedha.Gazeti la SCHWÄBISCHE ZEITUNG lina wasiwasi ikiwa kweli uchumi utasaidiwa iwapo kodi itashushwa.

Kwa maoni ya gazeti hilo uwekezaji na miradi ya kufufua uchumi ndio itakayozalisha nafasi za ajira na kuwanufaisha raia wa pato la wastani. Miradi ya aina hiyo ndio itakayosaidia kuleta faida zaidi na sio mipango ya muda mfupi tu.Kwa hivyo serikali lazima iwe tayari kutoa fedha za kutosha kusaidia uchumi na haraka ijadiliane masharti ya msaada utakaotolewa.

Mada nyingine inahusika na rais-mteule wa Marekani Barack Obama. Gazeti la NEUE OSNABRÜCKER ZEITUNG linasema:

Hadi hivi sasa yaonekena kuwa rais ajae wa Marekani katika kuunda serikali yake anawaleta pamoja wanasiasa wazoefu,wataalamu na wenye mawazo mapya.Hapo Obama anatumia uerevu.Yaonekana kuwa mwanasiasa huyo ametambua kwamba serikali,sawa na timu ya spoti inahitaji kuwa na wajuzi wanaojiamini.