Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani afanya ziara ya ghafla Afghanistan
29 Agosti 2010Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Karl-Theodor zu Guttenberg pamoja na Spika wa Bunge la Ujerumani, Norbert Lammert wamefanya ziara ya ghafla nchini Afghanistan. Viongozi hao wawili leo asubuhi walihudhuria ibada iliyofanyika Kunduz ya kuwakumbuka wanajeshi wa Ujerumani waliouawa nchini humo.
Viongozi hao pia walipewa taarifa kuhusu kikosi kipya cha kutoa mafunzo kitakachoanza kazi mwezi ujao wa Septemba na baadaye leo wanatarajiwa kuelekea kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Kabul.
Wakati huo huo katika gazeti la Jumapili la Ujerumani, Bild am Sonntag, zu Guttenberg amesema anafikiria kujumuisha kipindi cha majaribio kwa wanajeshi ambao watajiunga na jeshi la Ujerumani.
Katika miezi sita ya mwanzo, wanajeshi hao wapya huenda wakajitoa kwa urahisi, hatua ambayo amesema inaweza kulifanya jeshi kuwa la kuvutia zaidi. Mageuzi hayo yatakuwa ni sehemu ya mpango wa zu Guttenberg wa kupunguza ukubwa wa jeshi la Ujerumani kwa theluthi moja.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (DPAE/RTRE)
Mhariri: Mohammed Dahman