090309 Jung Afghanistan
9 Machi 2009
Waziri wa ulinzi wa serikali kuu ya Ujerumani,Franz Josef Jung ameondoka Ujerumani jana Jumatatu kuelekea kaskazini mwa Afghanistan, kuwatembelea wanajeshi wa Ujerumani. Hadi kesho Jumatano,waziri Jung anatazamiwa kuitembelea miji ya Termez huko Uzbekistan, Masar-e Sharif, Feyzabad na Kunduz nchini Afghanistan.
Serikali kuu ya Ujerumani inafuatilia kwa makini na kwa matumaini makubwa.Inajiwekea matumaini katika ujenzi mpya wa Afghanistan;hofu zinakutikana katika ile hali kwamba kwa muda mrefu jumuiya ya kimataifa ilikua ikitanguliza mbele mambo ambayo sio nchini Afghanistan.Ndio maana mafunzo kwaajili ya askari polisi yamekua yakiendelea kidogo kidogo tuu,Ujerumani ilipokua ikiyasimamia.Hivi sasa lakini jumuia ya kimataifa inahimiza askari polisi na wanajeshi wapatiwe mafunzo.
Hata Ujerumani imetathmini upya msimamo wake na kujishughulisha hivi sasa sio tuu na kuwapatia mafunzo askari polisi bali pia vikosi vya ulinzi.Katika mkutano wa usalama uliofanyika mjini Munich,waziri wa ulinzi Franz Josef Jung alifafanua yaliyofikiwa na kusema:
"Jumuiya ya kimataifa, tumewapatia mafunzo wanajeshi 70 000 wa kiafghanistan, kwa hivyo tunatakiwa tuwapatie mafunzo wanajeshi 65 wa ziada. Na tumewapatia mafunzo, kama sijakosea, askari polisi 35 elfu. Kwa hivyo hata katika suala hilo kuna upungufu wa askari polisi laki moja."
Hii leo waziri wa ulinzi wa serikali kuu ya Ujerumani Franz Josef Jung atakitembelea kituo cha polisi cha kufanayia mazowezi huko Masar-e-Shariff.Mada kuu wakati wa ziara yake hii inayoanza leo inahusu namna ya kuishirikisha Pakistan katika utaratibu wa kutuliza hali ya mambo katika eneo hilo.Mkakati wa kivitendo unahitajika anasema waziri wa ulinzi Franz Josef Jung:
""Pakistan,bonde la Swat na maeneo ya kikabila,yote hayo yamegeuzwa ngome na wataliban ,na pia ni maeneo wanakoandikishwa magaidi ambao baadae wanavuka mpaka na kuingia Afghanistan.Tunabidi tuzidishe na kuimarisha juhudi zetu hasa katika maeneo ya mpakani na kwa ushirikiano pamoja na Pakistan."
La maana lingekua pia kujaribu kusaka njia za kuzungumza na wataliban wanaofuata msimamo wa wastani.Rais Barack Obama wa Marekani ameshazungumzia uwezekano huo.
Wataliban ni mtihani mkubwa unayoyatikisa majimbo yasiyopungua kumi ya Afghanistan.Hata rais Hamid Karsai amekua akionya katika mkoa wa Helmand muongozo wa serikali kuu unafuatwa kwa sehemu tuu,katika mji mkuu na katika wilaya mbili;katika maeneo yaliyosalia ya mkoa huo, wataliban ndio wenye usemi.
Katika mikoa hiyo ya kusini ndiko rais wa Marekani Barack Obama anakopanga kutuma wanajeshi 17 elfu wa ziada.Anakiri hata hivyo mtutu wa bunduki sio njia ya kupatikana ushindi nchini Afghanistan.
Ujerumani imetuma wanajeshi 3700 kaskazini mwa Afghanistan.Na ingawa wanatambuliwa na kukubalika miongoni mwa jamii,hata hivyo na wao pia wanakua kila wakati wanahujumiwa.Ndio maana kuna haja ya kutumwa wanajeshi ziada wa Ujerumani kuimarisha nguvu za kikosi cha kuingilia kati haraka ili kukilinda vyema zaidi kituo cha wanajeshi cha Kunduz.Hata hivyo waziri wa ulinzi wa serikali kuu ya ujerumani anasema wanajeshi hao ziada hawatapindukia 4500.
Serikali kuu ya Ujerumani inasema wanajeshi wa shirikisho Bundeswehr wataendelea kuwepo kaskazini mwa Afghanistan,ikisubiriwa kuonekana tija itakayotokana na sera za serikali mpya ya Marekani kuelekea Afghanistan.