Waziri wa nje wa Marekani Hillary Clinton ziarani katika Ghuba
15 Februari 2010Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Hillary Clinton yuko ziarani mjini Ryadh katika juhudi za kuitanabahisha Saud Arabia iunge mkono vikwazo ziada dhidi ya Iran.Lengo kama hilo analifuata pia waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mjini Moscow.
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Hillary Clinton akiwa ziarani katika eneo la Ghuba kusaka uungaji mkono wa mataifa hayo kwa mpango wa Marekani wa kuiwekea vikwazo ziada Iran kutokana na mradi wake unaotatanisha wa kinuklea,amesema "majirani wa Iran wana kila sababu ya kuingiwa na hofu kutokana na dhamiri za kinuklea za jamhuri ya kiislam."
Akizungumza na wanafunzi mjini Doha leo asubuhi,waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani amehakikisha nchi yake haijapanga kutumia nguvu dhidi ya Iran ili iachane na kiu cha kinuklea,lakini inapendelea kuzidisha shinikizo la kimataifa kupitia baraza la usalama la umoja wa mataifa.
Shinikizo hilo"litayahusu zaidi makampuni yanayomilikiwa na walinzi wa mapinduzi wanaotaka kuivunja nguvu serikali ya Iran akihoji "Iran inaelekea kugeuka utawala wa kiimla wa kijeshi."
Akizungumza na waandishi habari ,akiwa njiani kuelekea Ryadh-kituo cha pili cha ziara yake ya Ghuba,waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani amesema walinzi wa mapinduzi ya kiislam-Pasadran wanadhibiti sekta zote muhimu za kiuchumi na kwamba wao ndio wanaobeba dhamana ya mradi wa kinuklea.
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani amesema:
"Iran haiiachii jumuia ya kimataifa fursa nyengine isipokua kulazimisha hatua zichukuliwe dhidi ya uchokozi wake.Kwa pamoja tunaihimiza Iran idurusu uamuzi wake wa hatari.Tunashirikiana moja kwa moja na washirika wetu wa kimkoa na kimataifa kuona njia inayobidi kufuatwa,kuandaa na kutia njiani hatua mpya ili kuitanabahisha Iran ibadilishe mkondo wake."
Mjini Ryadh waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani amepangiwa kuonana na waziri mwenzake,mwanamfalme Saoud Al Faysal,kabla ya kuzungumza na mfalme Abdallah Ibn Abdul Aziz.
Suala hilo hilo la Iran ndio chanzo cha ziara ya waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mjini Moscow hii leo.
Benjamin Netanyahu amekutana na rais Dmitri Medvedev na kesho amepangiwa kukutana na waziri mkuu Vladimir Putin.
Ikulu ya Urusi ilithibitisha taarifa iliyotolewa hapo awali na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kwamba kadhia ya Iran na mradi wake wa kinuklea ni miongoni mwa mada mazungumzoni.
Mwandishi:Hamidou,Oummilkheir/ AFP
Imepitiwa na:Abdul-Rahman,Mohammed