1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa mazingira wa Ujerumani azuru Kenya

Yusra Buwayhid
28 Septemba 2016

Waziri wa mazingira wa Ujerumani, Barbara Hendricks, amewasili nchini Kenya kwa ziara ya siku nne, huku Kongamano la Kupambana na Biashara Haramu ya Viumbe Vilivyo Hatarini, CITES, linaendelea nchini Afrika Kusini.

https://p.dw.com/p/2QgRF
Berlin Bundestag Umwelt Ministerin Barbara Hendricks zu Klimaabkommen
Picha: Getty Images/AFP/O. Andersen

Katika ziara yake hiyo, Hendricks, atakutana na wakurugenzi watendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa makazi, UN-Habitat pamoja na Shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa UNEP mjini Nairobi.

Na Septemba 30, waziri huyo anategemewa kuhudhuria sherehe za siku ya kitaifa ya Ujerumani zitakazofanyika katika ubalozi wa Ujerumani mjini Nairobi, huku Bwana Charles Sunkuli, Katibu Mkuu wa idara ya mazingira ya Kenya akiwa mgeni rasmi.

Baada ya hapo, mnamo Octoba mosi Hendricks atatembelea miradi mbalimbali inayoendeshwa katika mbuga za wanyama nchini Kenya, ikiwa ni pamoja na mradi wa "Elerai" - unaotoa mafunzo kwa walinzi wa mbuga za wanyama pamoja na kukuza mashirikiano na upande wa nchi jirani ya Tanzania - wa Shirika la Kulinda Wanyama Pori Afrika AWF, ambao Wizara ya Mazingira ya Ujerumani imekuwa ikiunga mkono. Waziri huyo wa Mazingira wa Ujerumani pia atakutana na baadhi ya walinzi wa wanyama pori.

Nchi za Kiafrika zimegawanyika katika suala la biashara ya pembe za ndovu na vifaru, lakini Kenya pamoja na Ujerumani ni miongoni mwa nchi zinazopinga hatua hiyo.

Südafrika CITES in Johannesburg
Kongamano la CITES mjini Johannesburg, Afrika KusiniPicha: DW/B. Bascomb

Kabla ya kuanza ziara yake hiyo, waziri Hendricks alisema Ujerumani katu haitounga mkono suala la kuondoa marufuku dhidi ya biashara hiyo.

"Tutaendelea kusisitiza kuwepo marufuku ya biashara ya pembe za ndovu na vifaru. Hasa ikizingatiwa kwamba ujangili umezidi kukithiri na umeshindwa kudhibitiwa, kuregeza kamba juu ya suala hilo ni kosa kubwa. Ujerumani inapinga mapendekezo yaliyowasilishwa na Swaziland kuhusu biashara ya pembe za vifaru, Zimbabwe na Namibia juu ya pendekezo lao la kuanzisha tena biashara ya pembe za ndovu, pamoja na lile la Afrika Kusini juu ya kuanzisha mfumo rasmi wa biashara hiyo," amesema Hendricks.

Akiwa katika kongamano la CITES linaloendelea nchini Afrika Kusini, Hendricks aliwasilisha orodha kubwa ya data zinazorahisisha kuweza kutambua nchi asili zilipotokea pembe za ndovu. Ni utafiti uliofanywa Ujerumani kama moja wapo ya hatua za kusaidia kulinda wanyama walio hatarini hutoweka.

Aidha kwa upande wa misaada ya maendeleo, Kenya na Ujerumani zilifanya mazungumzo mwezi uliopita mjini Berlin, na Ujerumani imeahidi kutoa euro milioni 252.35 zitakazotumika kuendeleza miradi ya maendeleo kwa mwaka 2017/2018, ikiwa ni pamoja na mkopo wa euro milioni 100.

Fedha hizo zitatumika katika miradi ya kuleta maendeleo endelevu ya uchumi ikiwa ni pamoja na kukuza maendeleo ya vijana na kuwapatia mafunzo ya ufundi stadi. Aidha fedha hizo pia zitatumika katika masuala ya kilimo, maendeleo katika ya maeneo ya vijijini pamoja na kuimarisha sekta ya afya.

Halikadhalika, Ujerumani imeahidi kuisaidia Kenya kwa euro milioni 9 kama nchi ya barani Afrika iliyoelemewa na wakimbizi.

Misaada ya aina hii ni ya kwanza kati ya nchi hizo mbili, tokea Kenya ilipopata hadhi ya nchi ya kipato cha chini cha wastani.

 

Mwandishi: Yusra Buwayhid

Mhariri:Iddi Ssessanga