Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani azuru Mashariki ya Kati
8 Juni 2019Ziara ya waziri Heiko Maas nchini Iraq ilikuwa haikutangazwa katika ratiba ya safari yake kwa sababu za kiusalama. Mjini Baghdad anatarajiwa kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu Adel Abdel Mahdi, pamoja na Rais Batham Salih.
Akizungumza baada ya kuwasili Iraq, Maas amesema ''kuna kitisho cha dhahiri cha hatari isiyotabirika, inayoweza kutokana na kukadiria vibaya, uchokozi na kuelewa visivyo azma ya upande mwingine katika eneo hilo lenye mivutano mikali''.
Soma zaidi: Marekani haipingi mfumo wa biashara wa Ulaya kuisaidia Iran
Akitoka Iraq Jumapili, waziri huyo wa Ujerumani anatarajiwa kuendelea na ziara yake kwa kuzitembelea Umoja wa Falma za Kiarabu na Jordan, kabla ya kufika Iran ambako ni kilele cha ziara hiyo. Katika mazungumzo na viongozi wa Iran, Maas atapigia debe kuendelezwa kwa mkataba kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, uliosiniwa mwaka 2015 baina ya nchi hiyo na mataifa yenye nguvu duniani.
Ulaya kujitwisha jukumu la upatanishi
Heiko Maas ameelezea wasiwasi mkubwa kuhusu mvutano kati ya Marekani na Iran ambao amesema umefika katika kiwango cha kutisha, akisema ni jukumu la nchi za Ulaya kuongoza njia katika matika mazungumzo ya kuutanzua mzozo huo.
''Kupanuka kwa uhasama kunatulazimu sisi kama majirani wa nchi za Ulaya, kuingilia kati kuhimiza ustahimilivu na kuishi kwa amani.'' Amesema waziri Maas na kuongeza kuwa ulazima wa kusaka suluhisho unaongezeka pale tofauti zinapooneka kubwa kiasi cha kukosa suluhu, au pale mivutano inapofikia kilele.
Mwaka jana, Marekani ilichukuwa uamuzi wa peke yake wa kujiondoa katika mkataba kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, ambao ulilenga kuizuia nchi hiyo kuunda silaha za atomiki, na imeanza kutekeleza vikwazo vikali dhidi ya sekta za mafuta na za kibenki za Iran, ambavyo vimeulemaza uchumi wa taifa hilo la Kiislamu.
Uamuzi wa Marekani waziacha nchi za Ulaya mahali panapoteleza
Hatua hiyo ya Marekani imeziacha katika hali ngumu nchi za Ulaya ambazo zinataka kuudumisha mkataba huo.
Mwezi uliopita, rais wa Iran Hassan Rouhani alizipa nchi hizo za Ulaya muda wa siku 60 kuiondolea vikwazo nchi yake, la sivyo itaanza kurutubisha tena madini ya urani.
Maas amesema Ulaya inaamini kwa dhati kwamba kila juhudi inahitajika kuhakikisha kuendelea kuwepo kwa mkataba huo uliosainiwa mjini Vienna.
Wakati mvutano ukishamiri kwenye Ghuba ya Uajemi, Marekani imeishutumu Iran kuhusika na mashambulizi dhidi ya meli nne za kubeba mafuta, zilizokuwa zimetia nanga kwenye bandari ya Fujirah katika Umoja wa Falme za Kiarabu mwezi uliopita. Iran imekanusha shutuma hizo, ambazo imesema zinalenga kuzidisha uhasama katika ukanda huo tete.
Soma zaidi: Marekani yasema inataka kuizuia Iran, si vitai:
Kuna hofu kwamba mvutano huo baina ya Marekani na Iran unaweza kuenea hadi nchini Iraq, ambako yapo makundi wa wanamgambo wa Kishia wanaosaidiwa na Iran. Iraq inazo pia kambi za Marekani zenye maelfu ya wanajeshi wanaoisaidia Iraq katika mapambano dhidi ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS.
dpae, ape