1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaChina

Waziri wa Mambo ya nje wa China Qin Gang aondolewa mamlakani

25 Julai 2023

Waziri wa mambo ya nje wa China Qin Gang amefukuzwa kazi siku ya Jumanne baada ya kutoonekana hadharani kwa mwezi mmoja bila maelezo yoyote kutolewa na Chama tawala cha Kikomunisti.

https://p.dw.com/p/4UNxi
Außenminister China Qin Gang | in Berlin
Picha: Thomas Trutschel/photothek/picture alliance

Kitendo cha kutoonekana kwa Qin kilizua uvumi kwamba kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 57, anayechukuliwa kuwa karibu na Rais Xi Jinping, amekuwa akikabiliwa na uchunguzi au kutengwa na utawala wa sasa.

Hapo awali, wizara ya mambo ya nje ya China ilitaja kuwa ukimya wa Qin ulitokana na sababu za kiafya, lakini hivi majuzi wizara hiyo ilikataa kutoa taarifa zozote licha ya kuhojiwa mara kwa mara. 

Chombo cha habari cha serikali Xinhua kimesema Jumanne jioni kwamba bunge kuu la China lilipiga kura ya kumuondoa Qin Gang madarakani na nafasi yake kuchukuliwa na Wang Yi.

Xinhua haikutoa sababu ya kuondolewa kwa Qin lakini imesema Rais Xi alitia saini nyaraka ya uamuzi huo.

China | US Außenminister Blinken in China
Rais wa China Xi JinpingPicha: Leah Millis/Pool/REUTERS

Alipoulizwa siku ya Jumanne kuhusu Qin, msemaji wa wizara ya mambo ya nje Mao Ning aliwaambia waandishi wa habari kwamba hana taarifa za kuwapa na kusisitiza kwamba shughuli za kidiplomasia za China hubadilika kwa kasi.

China imekuwa ikikaa kimya kwa wiki kadhaa kuhusu hatima ya Qin, ambaye hajaonekana hadharani tangu Juni 25,2023 alipokutana na naibu waziri wa mambo ya nje wa Urusi Andrey Rudenko mjini Beijing.  

Soma pia: China yashindwa kumtuma waziri wake wa nje Indonesia

Kutohudhuria kwake katika mkutano wa ngazi ya juu wa nchi za mataifa wanachama wa Jumuiya ya Kusini Mashariki ya Asia ASEAN nchini Indonesia wiki mbili baadaye kulizua taharuki, huku afya ya Qin ikitajwa kuwa sababu.

Hata hivyo, hiyo haikusaidia sana kuzuia kuenea kwa uvumi mtandaoni, ambao baadhi ulidai Qin alikuwa chini ya uchunguzi rasmi kwa madai ya kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mtangazaji maarufu wa televisheni.

Tahadhari kabla ya kutoa maoni juu ya mabadiliko hayo.

Chinas Außenminister Qin Gang (l.) und Wang Yi
Kutoka kushoto: Waziri Qin Gang alieondolewa madarakani akiwa pamoja na Wang Yi aliyechukua nafasi yake.Picha: Sergei Karpukhin/picture alliance/dpa/TASS

Neil Thomas kutoka Taasisi ya Sera ya Jumuiya ya Asia, ambacho ni chombo cha wasomi cha Marekani ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa Twiter kuwa Qin atasalia hata hivyo katika nafasi yake ya juu zaidi kama Mshauri wa Serikali. Thomas amesema kwa hivyo hana uhakika wa asilimia mia moja kuwa Qin kafurushwa kwa kuwa hatakiwi na uongozi wa sasa.

Mwezi uliopita, majukumu mengi ya Qin yalitekelezwa na Wang, mwanadiplomasia mkuu wa China ambaye anaongoza sera ya mambo ya nje ya Chama tawala cha Kikomunisti na hivyo kuwa juu ya Qin katika ngazi ya serikali. Qin alichukua wadhifa huo kutoka kwa Wang kama waziri wa mambo ya nje mwezi Desemba mwaka jana.

Kutoonekana kwa Qin katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita kuliacha ombwe katika wadhifa wa waziri wa mambo ya nje wa China. Ziara mjini Beijing ya mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell na ile ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza James Cleverly ziliahirishwa kutokana na hali hiyo.

Qin ambaye alikuwa mzungumzaji mzuri wa Kiingereza, alichukuliwa kama kioo cha China mjini Washington kupitia mikutano ya hadhara na vyombo vya habari ambapo alitetea msimamo wa kisiasa wa China. Awali, alikuwa msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China, ambapo alijizolea umaarufu kwa kujibu maswali magumu ya waandishi wa habari.

(AFPE)