1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa mambo ya nje Ujerumani aanza ziara Marekani

5 Januari 2022

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock ameondoka leo Jumatano kuelekea nchini Marekani anakotarajiwa kufanya mazungumzo yatakayoangazia hali ngumu ya uhusiano kati ya mataifa ya Ulaya na Urusi.

https://p.dw.com/p/45Bc5
Deutschland Berlin | Annalena Baerbock, Außenministerin zu Afghanistan
Picha: Michael Sohn/AP Photo/picture alliance

Hii ni ziara ya kwanza ya bibi nchini Marekani tangu alipochukua wadhifa huo katika serikali mpya nchini Ujerumani. 

"Kadri nyakati zinavyozidi kuwa ngumu, ndivyo nguvu ya ushirikiano pia inazidi, na sisi watu wa bara la Ulaya, hatuna mshirika thabiti zaidi ya Marekani,” Baerbock amesema alipokuwa akiondoka Berlin.

Anatarajia kukutana na waziri mwenza wa Marekani, Antony Blinken, ambae alikutana nae mara ya mwisho kwenye mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa kundi la G7, mkutano uliofanyika mjini Liverpool mwezi Disemba mwaka jana, muda mfupi baada ya serikali mpya ya muungano kuapishwa.

Wanadiplomasia hao wawili wanatarajiwa kujadili kuhusu kitendo cha hivi karibuni ambapo Urusi imeongeza wanajeshi karibu na mpaka wake na Ukraine, na kusababisha hofu katika nchi za Magharibi kwamba Moscow huenda inapanga uvamizi. Baerbock amesema Ulaya na Marekani zimekuwa na ujumbe wa pamoja kwamba "Hatua ya Urusi itakuwa na athari za wazi, na kwamba njia pekee ya kumaliza mgogoro ni mazungumzo."

Akizungumza na waandishi wa habari, msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Ujerumani Christopher Burger amesema mazungumzo ya huko Washington yatahusu mambo kadha wa kadhaa.

soma zaidi:Mawaziri wa G7 wakutana Brussels kuijadili Urusi

Moscow imekuwa ikionywa mara kwa mara katika wiki zilizopita dhidi ya harakati zozote za kijeshi, na Washington, NATO na washirika mbalimbali. Hata hivyo, Baerbock amebainisha kuwa hali imefikia "awamu nyeti, na kwamba mazungumzo muhimu yanaendelea katika ngazi tofauti.

Mkutano wake unakuja kabla ya mazungumzo yaliyopangwa kati ya Ukraine, Urusi, Ujerumani na Ufaransa juu ya mgogoro wa Ukraine huko Moscow siku ya Alhamisi. Wanadiplomasia wa Urusi na Marekani pia wamepangwa kukutana mjini Geneva siku ya Jumatatu na Jumanne wiki ijayo huku Urusi na NATO wakipanga mazungumzo tofauti Januari 12.

Katika ziara yake ya Washington, Baerbock pia amepangiwa kukutana na Spika wa Bunge la Marekani Nancy Pelosi.

Mkutano wao unakuja katika mkesha wa kumbukumbu ya mwaka mmoja tokea Januari 6, 2021, wakati wafuasi wa Donald Trump waliposhambulia majengo ya bunge au Capitol ambalo ndilo mhimili wa utawala wa Marekani.

Chanzo: ap/afp