Waziri wa Kongo ataka kumkamata Kagame, akimwita "mhalifu"
26 Novemba 2024Waziri huyo akizungumza katika mji huo mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini, alitishia kumkamata Rais Paul Kagame na Wanyarwanda wote na Wakongo wanaomuunga mkono.
"Nchi yetu haitatawaliwa na Wanyarwanda kamwe. Muelewe vizuri kwamba tutawakamata, na Kagame mwenyewe tutamkamata pia. Nyinyi nyote mlioko katika mawasiliano na Wanyarwanda na Kagame, tutawahamishia katika gereza la kijeshi la Angenga," alisema waziri Mutamba.Kongo yaishitaki Rwanda kwenye Mahakama ya Afrika Mashariki
Mamlaka za Kongo, pamoja na Umoja wa Mataifa, zinaituhumu Rwanda kuunga mkono waasi wa M23wanaopigana na jeshi la kitaifa la Kongo.
Wataalamu wasema ni maneno matupu
Wachambuzi wa mambo wanaamini kwamba kauli ya Waziri Constant Mutamba ni maneno tu, na haiwezi kutekelezwa. Kulingana na Octave Nasena, wakili anayefanya kazi mjini Kinshasa, waziri wa sheria wa Kongo hana mamlaka ya kutoa hati ya kumkamata rais wa nchi nyingine.
Soma: M23 waukamata tena mji wa Kalembe mashariki ya Kongo
Anasema, "Mzozo kati ya Rwanda na Kongo-Kinshasa ni suala la kisiasa, si la kisheria. Kila kitu cha kisiasa kinapaswa kushughulikiwa kisiasa, na kila kitu cha kisheria kinapaswa kushughulikiwa kisheria. Ni katika ngazi ya kisiasa tu ambapo Kagame anaweza kukamatwa. Hayo ni majukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC ambayo ni chombo cha kisheria."
Baada ya kauli za kushangaza za Waziri Constant Mutamba, majibu ya serikali ya Rwanda hayakuchelewa. Yolande Makolo, msemaji wa serikali ya mjini Kigali, alilaani alichokiita "uchochezi wa hali ya juu." Alionya dhidi ya uwezekano wa kuhusika kwa wahalifu na wafungwa katika vikosi vinavyopigana pamoja na jeshi la Kongo.Msemaji wa jeshi la Kongo asema jeshi limeurejesha mji wa kalemba kwenye udhibiti.
Kudorora kwa Mahusiano kwa Muda Mrefu
Nkere Ntanda, profesa katika Chuo Kikuu cha Kinshasa, anahofu kwamba kudorora kwa mahusiano kati ya majirani hao wawili kutakuwa kwa muda mrefu: "Mahusiano kati ya Kongo na Rwanda si mazuri, na matamshi kama haya hayaashirii kuwa suluhisho litapatikana hivi karibuni. Ni dhahiri kuwa nafasi za kurejesha mahusiano mazuri kati ya Kinshasa na Kigali ni ndogo sana kwa sasa."
Kwa zaidi ya miaka miwili, waasi wa M23 wamekuwa wakishikilia maeneo kadhaa ya jimbo la Kivu Kaskazini. Mamlaka za Rwanda zinakanusha tuhuma za kuliunga mkono kundi hilo.