1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa kigeni wa Kenya azuru Ujerumani

Josephat Nyiro Charo7 Februari 2014

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Kenya, Amina Mohamed, anazuru Berlin, Ujerumani. Jana (06.02.2014) alikutana na viongozi wa makampuni na mashirika ya kibiashara na kusisitiza umuhimu wa uwekezaji Kenya.

https://p.dw.com/p/1B4ql
Kenia Außenministerin Amina Mohamed Deutsche Industrie- und Handelskammer
Waziri wa mambo ya kigeni wa Kenya, Amina MohamedPicha: DW/J. Charo Nyiro

Akizungumza kwenye mkutano uliondaliwa na shirika la Ujerumani linaloshughulikia ushirikiano na bara la Afrika, waziri Amina Mohammed alisema Kenya imefungua milango yake kwa Ujerumani kufanya biashara kwa kuwa ndiyo iliyokuwa nchi ya kwanza kuutambua uhuru wa Kenya mnamo mwaka 1963. Amedokeza kwamba kampuni ya Ujerumani ya Bosch tayari imefungua ofisi yake jijini Nairobi wiki iliyopoita, ishara kwamba kampuni za Ujerumani zina imani na mazingira ya kibiashara katika taifa hilo.

Huku akiwashawishi Wajerumani kwenda kuwekeza nchini Kenya, Bi Mohamed amekiri kuna changamoto za kiusalama zinazowatia hofu wawekezaji wa kigeni. Akizungumza na idhaa hii kuhusu changamoto hizo ametoa mfano wa hali ya wasiwasi iliyojitokeza katika mji wa bandari wa Mombasa mapema wiki hii ambapo maafisa wa polisi walikabiliana na vijana wa kiislamu waliokuwa katika msikiti, ikisemekana walikuwa wakipokea mafunzo wawe na itikadi kali za kidini ili wajiunge na makundi ya kigaidi.

"Magaidi hawajui mipaka. Wameshawahi kuishambulia Kenya na Tanzania. Nadhani kuna haja ya kushirikiana kutoa taarifa za kijasusi na kujenga uwezo kuhakikisha tunawashinda kila mara wanapopanga njama ya kushambulia. Tukio la Mombasa ni mfano wa ufanisi wa serikali kuzuia kitu ambacho kingekuja kuwa hatari."

Hata hivyo amesema changamoto za kiusalama si kubwa na zimedhibitiwa. "Matatizo yanatokea nchi jirani. Unaweza kuchagua marafiki lakini huwezi kuchagua majirani. Kwa hiyo kunatakiwa kuwepo ushirikiano katika kubadilishana taarifa za kijasusi ili kukabiliana na maadui," akaongeza kusema waziri huyo.

Festnahmen und Haft nach Krawallen in Moschee in Mombasa
Vijana waliokuwa msikitini MombasaPicha: Reuters/Joseph Okanga

Wajerumani wawekeze katika miradi

Amewataka Wajerumani kuwekeza katika sekta ya madini, gesi na mafuta ambayo yamegunduliwa kaskazini mwa Kenya, na pia akitoa mfano wa mradi wa uchimbaji wa madini ya titanium huko Kwale katika jimbo la pwani. Amehimiza pia wawekezaji wa Kijerumani wajitokeze kuchukua nafasi katika mradi mkubwa wa ujenzi wa jiji la teknolojia ya kisasa la Konza, mradi ulio kwenye ekari 5,000 za ardhi kilomita 60 kutoka mji mkuu, Nairobi.

Waziri Amina Mohammed amezungumzia pia mradi mkubwa wa ujenzi wa barabara itakayoiunganisha bandari ya Lamu nchini Kenya hadi Douala nchini Cameroon na kuzitaka kampuni na mashirika ya Ujerumani kuwekeza katika mradi huo. Barabara hiyo itapitia Juba, mji mkuu wa Sudan Kusini, na Bangui, mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Akizungumza kuhusu ziara ya Bi Mohamed, Heiko Schwiderowski wa shirika la viwanda la Ujerumani, lililomualika katika ofizi zake jijini Berlin, DIHK, amesema, "Tunafurahia sana kwamba waziri Aminja liweza kututembelea katika shirika letu licha ya mualiko kuchelewa. Kenya ina umuhimu mkubwa kwetu kwetu, tuna ofisi yetu huko na kuna nafasi kubwa na kibiashara nchini humo. Kwa hiyo lilikuwa jambo la maana kuweza kuzungumza na waziri ana kwa ana."

Hapo jana pia waziri Amina Mohammed alikutana na waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Frank Walter Steinmeir, huko Berlin, ambapo walizugumzia masuala mbali mbali yenye umuhimu mkubwa kwa masilahi ya nchi zao, yakiwemo maendeleo ya kiuchumi na vipi Ujerumani inavyoweza kuchangia kuimarisha ukuaji uchumi na maendeleo katika kanda ya Afrika Mashariki na Kati.

Mwandishi: Josephat Charo

Mhariri: Mohammed Khelef