Waziri wa Ajira wa Ufaransa huenda akajiuzulu
12 Julai 2010Kashfa hiyo ni changamoto kali kabisa kwa serikali ya Rais Nicolas Sarkozy na leo usiku atahotubia taifa kwa njia ya televisheni katika jitahada ya kuituliza kashfa hiyo.
Kashfa hiyo imesababisha umaarufu wa Rais Sarkozy kupungua kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa tangu alipoingia madarakani mwaka 2007. Hata chama chake tawala cha UMP kinachofuata sera za kihafidhina kimefedheheshwa. Kashfa hiyo imechangia pia serikali kushindwa katika uchaguzi uliofanywa siku ya Jumapili kugombea kiti cha mbunge katika mtaa uliokuwa ukidhibitiwa na chama cha UMP.
Ni matumaini ya Rais Sarkozy kuwa leo usiku atakapotoa hotuba yake ya taifa kupitia televisheni, atafanikiwa kuizima kashfa hiyo na kurejea katika mipango yake ya kurekebisha mfumo wa malipo ya uzeeni. Waziri wake wa ajira,Eric Woerth anashughulikia mageuzi hayo.
Waziri huyo ndio anaetuhumiwa kupokea mchango wa Euro 150,000 kutoka kwa mwanamke tajiri kabisa nchini Ufaransa, Lilliane Bettencourt, anaemiliki kampuni ya vipodozi ya LÓreal. Inadaiwa kuwa waziri huyo alipokea fedha hizo, wakati wa kampeni ya uchaguzi wa rais uliogombewa na Sarkozy mwaka 2007.
Bibi Bettencourt mwenye umri wa miaka 87, ni mmojawapo wa matajiri waliofaidika sana kwa nafuu ya kodi iliyoidhinishwa na Sarkozy baada ya kushinda uchaguzi huo. Bettencourt alirejeshewa Euro milioni 30 kama nafuu ya kodi.
Wakati huo, Woerth alikuwa waziri wa bajeti akaiwa pia na dhamana ya kuzuia ukwepaji wa kodi. Wakosoaji wake wanauliza iwapo alitumia vibaya madaraka yake ili kumkinga Bettencourt dhidi ya ukaguzi wa kodi. Waziri Woerth amekanusha kupokea fedha zo zote kinyume na sheria. Na ripoti iliyotolewa haraka hiyo jana na serikali, imesema, hakuna uashahidi wo wote kuwa waziri huyo aliingilia kati kumlinda Bettencourt dhidi ya ukaguzi wa malipo ya kodi.
Hata hivyo, waziri Woerth hii leo amesema kuwa anafikiria kujiuzulu kama mweka hazina wa chama cha UMP ili kujiepusha na dhana ya kuwepo mgongano wa maslahi, kati ya dhima yake ya kukusanya michango ya chama na kama kiongozi serikalini. Wafuasi wa Sarkozy wanasema mada hiyo imeshamalizika, lakini wapinzani wa serikali wanashikilia kuwa bado kuna masuala mengi yanayongojea jawabu.
Mwandishi:P.Martin/AFPE/RTRE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman