Waziri von der Leyen ziarani Afghanistan
13 Desemba 2014Waziri huyo Ursula von der Leyen amewasili Jumamosi asubuhi katika kambi ya vikosi vya Ujerumani ilioko katika jimbo la Mazae -i-Sharif kaskazini mwa Afghanistan ambayo ndio kambi kubwa kabisa ya jeshi la Ujerumani ilioko nje ya nchi.
Katika ziara yake ya tatu nchini Afghanistan tokea ashike wadhifa huo mwaka jana na ikiwa zimebakia siku chake kabla ya kuondolewa kwa kikosi cha mapambano cha Jumuiya ya Kujihami ya NATO, von der Leyen ameonya dhidi ya kuondolewa kwa pupa nchini humo kwa kikosi hicho cha kimataifa.
Akizungumza akiwa ndani ya ndege kuelekea Afghanistan kwa ziara hiyo ya ghafla kuvitembelea vikosi vya Ujerumani vilioko Mazar-i-Sharif ,amesema jumuiya ya kimataifa imepata mafanikio makubwa nchini Afghanistan lakini hali nchini humo bado ni tete.
Mwanasiasa huyo wa chama cha Kansela Angela Merkel cha CDU amesema kundi la waasi wa Taliban litajaribu kuzidi kuiyumbisha nchi hiyo kwa kuzishambulia taasisi za kiraia na usalama hususan wakati huu NATO ikikamilisha harakati zake za mapambano za miaka 13 nchini humo.
Uondowaji wa majeshi uwe kwa hatua
Von der Leyen angependelea uondowaji wa kikosi hicho uwe wa hatua kwa hatua badala ya kuondolewa kwa mara moja kutoka katika nchi hiyo ilioathiriwa na vita.
Amekaririwa akisema "ni jambo la kuvutia sana jinsi nchi hiyo ya kijasiri inavyoendesha mapambano yake.".
Kuna kama wanajeshi 1,200 wa Ujerumani walioko nchini Afghanistan hivi sasa. Wakati shughuli za mapambano zitakapomalizika rasmi katika kipindi kisichozidi wiki mbili wanajeshi kama 850 wa Ujerumani wanatarajiwa kuendelea kubakia nchini humo kama sehemu ya kutowa mafunzo na ushauri kwa vikosi vya usalama vya Afghanistan katika kile kinachoitwa kuwa operesheni ya " Azma ya Kusaidia."
Kujifunza kutokana na Iraq
Ikiwa kama mfano wa tahadhari ni kuondolewa kwa haraka kwa vikosi vya Marekani nchini Iraq hapo mwaka 2011 baada ya nchi hizo mbili kushindwa kufikia Makubaliano juu ya hadhi ya vikosi vitakavyoendelea kubakia nchini humo.
Miaka mitatu baadae Rais Barack Obama wa Marekani baada ya kutafakari upya amelazimika kutuma tena vikosi vya Marekani nchini humo kuizuwiya nchi hiyo isitumbukie kwenye machafuko kutokana na kusonga mbele kwa wanamgambo wa kundi la Dola la Kiislamu wanaonyakuwa maeneo makubwa ya ardhi.
Hata Ujerumani inapanga kutuma mamia ya wanajeshi wa Ujerumani katika mji mkuu wa Arbil wa eneo lilioko chini ya mamlaka ya Wakurdi kaskazini mwa Iraq kutowa mafunzo kwa wapiganaji wa kikosi cha Wakurdi cha Peshmerga.
Ziara yatiwa kiwingu
Ziara ya waziri wa ulinzi wa Ujerumani imetiwa kiwingu baada ya mshambuliaji wa kujitowa muhanga kulishambulia jeshi na kusababisha maafa mjini Kabul Jumamosi ambapo awali afisa wa ngazi za juu wa mahakama alipigwa risasi na kuuwawa.
Katika mkoa wa Helmand wafanyakazi 12 wa kuteguwa mabomu wameuwawa na waasi wa Taliban wakati wanajeshi wawili wa Marekani nao wameuwawa karibu na kambi ya Bagram nje ya Kabul baada ya bomu kuripua msafara wa kijeshi.
Mapema hapo Alhamisi shambulio la kujitowa muhanga liliwauwa wanajeshi sita wa Aghanistan waliokuwemo ndani ya basi katika viunga vya mji huo. Hivi karibuni Taliban imekuwa pia ikiwalenga raia wa kigeni katika mashambulizi yao ambapo hapo Alhamisi Mjerumani mmoja aliuwawa katika shambulio dhidi ya Kituo cha Utamaduni cha Ufaransa mjini Kabul. Mlinzi wa usalama wa ubalozi wa Uingereza na familia moja ya Afrika Kusini pia walishambuliwa.
"Azma ya Kusaidia"
Takriban wanajeshi 12,000 kutoka nchi 40 wanatazamiwa kushiriki katika operesheni ya "Azma ya Kusaidia" itakayoongozwa na Jumuiya Kujihami ya NATO na Kikosi cha Kimataifa cha Usaidizi wa Usalama ISAF nchini Afghanistan.
Ujerumani inataka kuwa na wanajeshi 840 nchini humo baada ya kuidhinishwa na bunge Bundestag kabla ya Krismasi. Jeshi la Ujerumani ambalo linashughulikia usalama kaskazini mwa nchi hiyo jukumu lake jipya pia litakuwa katika mji mkuu wa Kabul na maeneo mengine manne ya nchi hiyo.
Kikosi hicho pia kitatumika katika kutowa usalama wa makampuni makubwa au wizara za serikali lakini hakitoshiriki katika harakati za mapambano lakini wanaweza kujihami wao wenyewe na washirika wao ikibidi hata kwa kutumia silaha.
Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/dpa. Reuters,AP
Mhariri : Iddi Ssessanga