Waziri Rice akutana na wajumbe wa vyama vya wafanyakazi Colombia
25 Januari 2008Matangazo
Waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani, Condoleezza Rice, na wabunge wa chama cha Democratic, wamekutana leo na wanachama wa vyama vya wafanyakazi nchini Colombia kutathmini ikiwa nchi hiyo iliyo hatari kwa uhuru wa vyama vya wafanyakazi, inastahili mkataba wa baishara huru. Hakuna maelezo yaliyotolewa kuhusu yaliyojadiliwa katika mkutano huo.
Condoleezza Rice amewasili mjini Medellin akiwa ameandamana na wabunge 10 wa Marekani katika juhudi za kuufufua mkataba huo uliosainiwa mara ya kwanza mnamo mwaka wa 2006 lakini ambao mpaka sasa bado haujaidhinishwa na bunge la Marekani.
Haitakuwa rahisi kwa Condoleezza Rice kulishawishi bunge la Marekani liupitishe mkataba huo hususan ikizingatiwa kampeni za kugombea urais zinazoendelea wakati huu nchini Marekani na Wamarekani wakikabiliwa na athari za kuyumba kwa uchumi wa nchi yao.
Wagombea wote watatu wa urais wa chama cha Democratic wanapinga kuiondolea vikwazo vya kibiashara Colombia.