Waziri Niebel ziarani Ethiopia
12 Januari 2011Jitahada za taasisi hizo za kiraia zitaweza kuleta maendeleo katika kanda nzima, ikiwa zitaungwa mkono na serikali. Waziri Niebel alitoa kauli hiyo alipokutana na waziri wa fedha wa Ethiopia Ato Sufian Ahmed mjini Addis Ababa. Vile vile amesema, ihakikishwe kuwa makundi yote ya kiraia yanashirikishwa ili kuweza kupiga vita umasikini na kuimarisha taasisi hizo za kiraia.Atafurahi ikiwa serikali ya Ethiopia,itaweza kuziamini zaidi sekta binafsi na taasisi za kiraia.
Mara kwa mara serikali hiyo inakosolewa na mashirika ya haki za binadamu kuhusu vikwazo vya kisheria vinavyoathiri kazi za mashirika yasio ya kiserikali, yanapohusika na masuala ya kuendeleza demokrasia na usawa.
Kwa mujibu wa "Human Rights Watch", shirika linalotetea haki za binadamu, serikali ya Ethiopia hutumia misaada ya maendeleo kuwakandamiza wapinzani, kwa kutoa huduma za kimsingi kwa wale wanaoiunga mkono serikali.Hata mtaalamu wa masuala ya bara la Afrika katika jumuiya inayoshughulikia makabila yalio hatarini kupotea, Ulrich Delius,amelalamika:
"Tunaamini kuwa serikali ya Ethiopia haikosolewi vya kutosha na jumuiya ya kimataifa, kunapotokea uvunjaji mkubwa wa haki za binaadamu, chini ya utawala wa sasa, kwani serikali hiyo inatazamwa kama msemaji muhimu wa masuala ya Afrika."
Wakati huo huo, waziri Niebel alipokutana na waziri mkuu wa Ethiopia Meles Zenawi alifurahi kusikia kuwa miongoni mwa vipaumbele katika sera za nchi hiyo ya Afrika Mashariki ni kuwasaidia wakulima wadogo wadogo. Wakati wa mazungumzo yao,waziri Niebel aliahidi kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na Ethiopia. Vile vile ameitaka serikali ya nchi hiyo kutoa msaada kwa makampuni binafsi.Kwani ukuaji wa kiuchumi wa kama asilimia 11 kwa mwaka, ni mzuri,lakini haukusaidia kuongeza nafasi za ajira. Kwa maoni ya Niebel, mazingira yanaweza kuboreshwa kuvutia uwekezaji wa kigeni.
Ethiopia ni nchi inayopokea msaada mkubwa wa maendeleo kutoka Ujerumani.Kati ya mwaka 2009 na 2011, Ujerumani imepanga kutoa jumla ya euro milioni 96. Msaada huo hasa ni kwa ajili ya kuendeleza miji,kugawa madaraka,kwa miradi ya kilimo na kuendeleza uchumi. Vile vile msaada mwingine wa euro milioni 18.5 ni kwa ajili ya kuhakikisha usalama wa chakula.
Mwandishi:Schadomsky,Ludger (Amharisch)/Prema Martin
Mpitiaji:Abdul-Rahman