Waziri mkuu wa Yemen anayeishi uhamishoni atembelea Aden
2 Agosti 2015Waziri mkuu wa Yemen Bahah aliwasili mjini Aden akiwa na mawaziri sita wa serikali jana Jumamosi (01.08.2015) na kuondoka siku hiyo hiyo, kwa mujibu wa mkuu wa uwanja wa ndege wa mjini Aden Tarek Abdu Ali.
Msemaji wa serikali ya Yemen iliyoko uhamishoni , Rageh Badie, amesema ziara ya Bahah ina lengo la kuweka hali ya kawaida kwa maisha ya watu mjini Aden. Amesema Bahah amefahamishwa juu ya hali ilivyo na utendaji wa serikali za mitaa, na kuongeza kwamba serikali inafanyakazi kurejesha huduma.
Badie amesema Bahah , ambaye pia ni makamu wa pili wa rais nchini Yemen , amefanya ziara ya mji huo na kuangalia uharibifu uliosababishwa na miezi ya mapigano.
Waziri mkuu atathmini uharibifu
Wakati huo huo , jeshi na wanamgambo wanaoiunga mkono serikali wamepata udhibiti wa mji muhimu upande wa kusini wa Zanjibar, maafisa wa usalama wamesema pamoja na watu walioshuhudia.
Ali Hawasah, kamanda anayeunga mkono serikali akizungumza kwa simu kutoka Zanjibar, amesema wapiganaji wake wameingia katika mji huo na wanawasaka wapiganaji wa Kihuthi. Ameongeza kuwa wapiganaji wanaoiunga mkono serikali wanasonga mbele wakipata msaada wa mashambulizi ya anga ya ndege za muungano unaoongozwa na Saudi Arabia huku kukiwa na mapigano makali na wapiganaji waasi.
Wapiganaji wanaoiunga mkono serikali wanalenga kupata udhibiti wa mji wa Zanjibar ili kuuweka mji wa Aden salama kutoka upande wa magharibi na kuzuwia njia muhimu ya kupata mahitaji kwa Wahuthi.
Maafisa wa Kihuthi wamesema wapiganaji wao wanaendelea kudhibiti eneo la magharibi na kusini la mji huo.
Mapigano yasambaa katika miji ya Yemen
Mapigano pia yameendelea katika mji wa tatu nchini Yemen wa Taiz, yakiuwa kiasi ya wapiganaji 65 kila upande katika muda wa siku mbili, maafisa wa hospitali na usalama wamesema.
Raia tisa pia wameuwawa mjini Taiz kutokana na mapigano hayo, maafisa hao wamesema.
Maafisa hao wamezungumza kwa masharti ya kutotajwa majina kwasababu hawana ruhusa ya kuzungumza na waandishi habari.
Muungano unaoongozwa na Saudi Arabia umekuwa ukifanya kampeni ya mashambulizi ya anga tangu Machi dhidi ya Wahuthi , ambao wanadhibiti mji mkuu Sanaa, sehemu za Yemen kaskazini na ambao wanajaribu kupanua eneo lao upande wa kusini wa taifa hilo masikini la Kiarabu lililoko katika rasi ya Arabuni.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape
Mhariri: Sudi Mnette