1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri mkuu wa Somalia Amejiuzulu

29 Oktoba 2007

Waziri mkuu wa Somalia Ali Mohamed Gedi amejiuzulu huku nchi hiyo ikizidi kutumbukia kwenye mzozo wa kisiasa.

https://p.dw.com/p/C7g5
Ali Mohamed Gedi
Ali Mohamed GediPicha: AP

Waziri mkuu Ali Mohamed Gedi amejiuzulu baada ya mvutano wa muda mrefu kati yake na rais wa mpito Abdullahi Yusuf.

Uamuzi huo wa bwana Gedi unatokea wakati ambapo katika mji mkuu wa Mogadishu raia wengi wanatoroka mapigano kati ya wapigananaji wenye msimamo mkali na majeshi ya serikali yanayoungwa mkono na Ethiopia.

Waziri mkuu huyo wa zamani aliwasilisha waraka wake wa kujiuzulu kwa rais Abdullahi Yusuf na mara moja rais Yusuf akamteuwa makamu wa bwana Gedi Salim Aliyow Ibrow kushikilia madaraka hayo.

Rais Yusuf aliwaeleza wawakilishi wa bunge kwamba amepokea kwa moyo mkunjufu uamuzi wa bwana Gedi na kwamba atajadili na wabunge kabla ya kumchagua waziri mkuu mpya.

Ali Mohamed Gedi mwenye umri wa miaka 55 alipanda hadi kufikia ngazi za juu katika serikali ya mpito ya Somalia mwaka 2004 lakini wamekuwa wakizozana na rais Yusuf mara kwa mara.

Waziri mkuu huyo wa zamani amesema amefikia uamuzi huo wa kujiuzulu baada ya kujadiliana na wafuasi wake pamoja na jamii ya kimataifa.

Rais wa mpito Abdullahi Yusuf hata hivyo kwa muda sasa amekuwa anashauriana na wabunge kuhusu kumng’oa bwana Gedi kutoka madarakani kwa sababu kuwa Gedi ameshindwa kumaliza makundi ya wanamgambo na pia kufanikisha katiba.

Wachambuzi pia wanamlaumu bwana Gedi kwa kuhusika zaidi na uamuzi wa kuwaleta wanajeshi wa Ethiopia nchini Somalia matokeo ambayo yamesabisha kuongezeka makundi ya wanamgambo.

Sababu nyingine kuu iliyomfanya bwana Gedi awe na wakati mgumu ni kutoka kwenye ukoo wake wa Hawiye ambao unadhibiti eneo kubwa la mji wa Mogadishu na pia ni ukoo mkubwa kabisa nchini Somalia.

Afisa mmoja katika ofisi ya waziri mkuu wa zamani Ali Mohamed Gedi amesema kuwa bwana Gedi anapendelea nchi yenye kufuata demokrasia, msimamo wa kadiri na uwazi lakini Somalia sasa inafuata mfumo wa taasisi isiyo heshimu sheria na kwamba mkataba wa serikali ya mpito unakabiliwa na dosari.

Mtalaam wa maswala ya siasa nchini Somalia kutoka kwenye taasisi ya siasa na jamii SWP Annette Weber anasema, kutokana na kushindwa kufaulu mkutano wa maelewano wa mwishoni wa wiki ni wazi kuwa Gedi ndie aliyekuwa anashikilia makali ya kisu huku upande wa pili ukiwa umeshikilia mpini na kwa hivyo wengi wanataka kuendelea kumtukuza rais Abdullahi Yusuf na hawataki kumlaumu kwa hali ya usalama inayozorota kila uchao ndio maana lazima angepatikana mtu atakae bebeshwa mzigo wa lawama.

Huku hayo yakiendelea hali ya usalama inazidi kuzorota nchini Somalia takriban watu kumi wameuwawa katika matukio tafauti.

Majeshi ya Somalia yakiungwa mkono na majeshi ya Ethiopia yanazidi kuingia ndani ya eneo la kusini kuwasaka wapiganaji wenye msimamo mkali.

Wakati huo huo Meli ya Japan iliyobeba shehena ya kemikali imetekwa nyara kaskazini mwa pwani ya Somalia, meli hiyo ina wafanyakazi 23 raia wa Korea, Mfilipino mmoja na raia mmoja wa Myanmar.