Waziri mkuu wa Myanmar afukuzwa kazi
20 Oktoba 2004Televisheni ya serekali huko Myanmar ilisema Jenerali Khin Nyunt, mwenye umri wa miaka 64, ameruhusiwa astaafu kwa sababu za kiafya. Mahala pake pamechukuliwa na Luteni-Jenerali Soe Win, M-Conservative aliye na umri wa katikati ya miaka ya hamsini, na anayetajwa kuwa msaidizi muaminfu wa mtu mwenye ushawishi mkubwa kabisa ndani ya baraza tawala la kijeshi, Than Shwe. Mataifa ya Kusini Mashariki ya Asia yaliokuwa yanaitetea Myanmar dhidi ya malalamiko ya nchi za nje kwamba iwachiwe iifuate ile ramani iliojichorea kuelekea dimokrasia, leo yalijitoa kimasomaso baada ya baraza la utawala wa kijeshi lenye msimamo mkakamavu nchini humo kuziondosha zile tamaa chache zilikuweko kwamba nchi hiyo huenda ikauona mwangaza wa diomokrasia. Hatua hiyo ya jana ilikuwa ni pigo kubwa katika juhudi za kuishawishi Myanmar ifanye marekebisho ya kisiasa kabla ya kuwa mwenyekliti wa Jumuiya ya Nchi za Kusini mashariki ya Asia, ASEAN, hapo mwaka 2006. Suala la nchi hiyo kuwa ya kidimokrasia ni sharti lililotolewa na nchi za Magharibi. Lakini mawaziri wa mambo ya kigeni wa nchi 10 za Jumuiya ya ASEAN wamejiepusha kutoa malalamiko ya moja kwa moja kwa watawala wa kijeshi wa Myanmar. Waziri wa mambo ya kigeni wa Indonesia, Hassan Wirajuda, aliwaambia waandishi wa habari kwamba hilo ni suala la mambo ya ndani ya Myanmar, lakini wao wanataraji kuteuliwa waziri mkuu mpya hakutaathiri vibaya matarajio ya kuweko mwenendo wa dimokrasia na masikilizano katika nchi hiyo. Hata hivyo, hana matumaini kwamba yule mwanaharakati wa dimokrasia katika Myanmar, Bibi San Suu Kyi, ataachiliwa karibuni kutoka kifungo cha nyumbani. Matumaini hayo yalikuweko wakati Jenerali Khin Nyunt alipokuwa madarakani.
Washirika wa Myanmar katika Jumuiya ya ASEAN wamekuwa hawalipi umuhimu sana suala la kuwekwa kizuizini Bibi Suu Kyi na kukandamizwa chama chake cha National League for Democracy, NLD, ambacho hakijaruhusiwa kuchukuwa madaraka baada ya kushinda kwa kishindo kikubwa chaguzi za mwaka 1990. Mpango wa Jenerali Khin Nyunt wa hatua saba kuelekea dimokrasia, ambao ulitangazwa mwaka jana, ulikusudia kufungua njia ya kuweko serekali ya kiraia katika nchi hiyo iliotawaliwa na serekali za kijeshi za sura mbali mbali tangu mwaka 1962. Lakini mtu mwenye nguvu katika baraza tawala la kijeshi katika nchi hiyo, Than Shwe, alikuwa mkakamavu hata kabla ya kuitishwa mkutano wa kutunga katiba mpya, ambao ulikuwa ni hatua ya kwanza ya ramani kuelekea dimokrasia, na akakataa kumwacha huru Bibi Suu Ky. Chama cha NLD baadae kiliususia mkutano wa katiba ambao wahakiki waliuita kuwa ni wa aibu.
Ilivokuwa Myanmar inatazamiwa kuwa mwenyekiti wa Jumuiya ya ASEAN hapo mwaka 2006 na kuwa mwenyeji wa mikutano baina ya jumuiya hiyo na nchi za Magharibi, nchi za Kusini Mashariki ya Asia zitakabiliwa na mbinyo mkubwa zaidi kutoka washirika wao wa kibiashara wa Ulaya na Marekani zichukuwe msimamo mkali zaidi dhidi ya Myanmar. Ndani ya Jumuiya ya ASEAN, ilio na msingi wa kutoingiliana katika mambo ya kila nchi mwanachama, kuna Indonesia, Philippines, Malaysia, Brunei, Singapore, Thailand, Vietnam, Laos, Cambodia na Myanmar. Kuna wachunguzi wanaosema kwamba Myanmar imewafikisha majirani zake karibu mwisho wa kuwa na subira, lakini hakuzungumziwi nchi hiyo kufukuzwa kutoka jumuiya hiyo.
Umoja wa Mataifa umesema una wasiwasi juu ya kufukuzwa kazi na kuwekwa kizuizini waziri mkuu Khin Nyunt, na katibu mkuu wa umoja huo, Kofi Annan, ana wasiwasi juu ya hali ya mwanaharaki wa kupigania dimokrasia katika nchi hiyo, Bibi San Suu Kyi. Msemaji wa Umoja wa Mataifa alitaka bibi huyo na makamo wake, Tin Oo, waachiliwe huru bila ya kuchelewa.
Pia Marekani haijajizuwia kuishambulia hatua hiyo ya watawala wa Myanmar na kuiita kuwa ni pigo kwa matarajio machache kwamba watawala wa nchi hiyo wangerejesha haki za kisiasa na za kibinadamu au wangefungua mdahala na kiongozi wa upinzani aliye kizuizini, Bibi Aung San Kyi.
Miraji Othman