Waziri Mkuu wa Mali ajiuzulu
11 Desemba 2012Tangazo la Cheick Modibo Diarra kujiuzulu wadhifa wake ambalo limerushwa na kituo cha taifa cha utangazaji, lilikuwa fupi. ''Mimi Cheick Modibo Diarra najiuzulu pamoja na serikali yangu'', alisema katika tangazo hilo katika sauti yenye unyonge. Aliwashukuru wanamuunga mkono na kuelezea matumaini kwamba atakayechukua nafasi yake atakuwa na mafanikio.
Ujumbe wake huo ulitolewa saa kadhaa baada ya taarifa kutoka kwa watu walio karibu naye, kwamba waziri mkuu alikuwa amekamatwa na wanajeshi 20 kutoka kambi ya Kati iliyoko nje kidogo ya mji mkuu, Bamako, ambayo ni makao makuu ya wanajeshi walioiangusha serikali mwezi Machi mwaka huu. Taarifa hizo zilidai kuwa wanajeshi hao walipewa amri na aliyekuwa kiongozi wa mapinduzi hayo, Kapteni Amadou Sanogo. Afisa mmoja wa usalama alithibitisha taarifa hiyo baadaye.
Mkono wa Kapteni Sanogo
Diarra alikuwa na mpango wa kwenda mjini Paris jana kwa matibabu, lakini alilazimika kuiahirisha safari hiyo baada ya kuarifiwa kwamba mzigo wake ulikuwa umetolewa ndani ya ndege ambaye ingemsafirisha. Maafisa walio karibu naye wamesema kuwa alikuwa amerekodi ujumbe mfupi ambao ungerushwa kwenye kituo cha taifa cha televisheni, lakini wanajeshi waliwahi kituoni humo na kuuchukua ujumbe huo.
Cheick Modibo Diarra aliteuliwa kuwa waziri mkuu wiki chache baada ya mapinduzi ya mwezi Machi ambayo yaliitumbukiza Mali, ambayo hapo awali ilikuwa na utawala imara wa kidemokrasia, katika mzozo ambao umesababisha sehemu yake kubwa ya kaskazini kuangukia mikononi mwa wanamgambo wenye itikadi kali ya kiislamu.
Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 60 anaunga mkono kuletwa kwa wanajeshi kutoka nchi za kanda ya Afrika magharibi, kusaidia kuwafukuza wanamgambo hao wanaoishikilia sehemu ya kaskazini. Kapteni Sanogo anaupinga vikali mpango huo.
Tofauti juu ya kuletwa vikosi vya nje
Kapteni Amadou Sanogo ambaye hakujulikana siku za nyuma, aliongoza mapinduzi yaliyoiangusha serikali ya rais Amadou Toumani Toure, wiki sita tu kabla ya uchaguzi ambao ungemaliza muda wake madarakani. Mapinduzi hayo yalifanyika wakati nchi ikikabiliwa na uasi wa watu wa jamii ya Toureg, ambao walitaka kujitenga na kujitangazia taifa lao huru lijulikanalo kama Azawad. Kupinduliwa kwa serikali kuliirahisisha kazi ya waasi hao, ambao walishirikiana na wanamgambo wa itikadi kali ya kiislamu wenye mafungamanao na mtandao wa al-Qaida.
Hata hivyo, makundi hayo sasa yamefarakana, na wanamgambo wa kiislamu ndio wanaoishikilia sehemu ya kaskazini baada ya kuwatimua watuareg. Nchi za Afrika Magharibi zinaliwekea shinikizo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuupitisha mpango wa kuingilia kijeshi kuikomboa kaskazini ya Mali, mpango ambao unaungwa mkono na Ufaransa.
Nchi za magharibi zinahofia kuwa sehemu hiyo inaweza kugeuka maficho ya makundi ya kigaidi. Umoja wa Ulaya jana uliafiki mpango wa kupelekwa kwa maafisa watakaotoa mafunzo kuisaidia Mali kulirejesha eneo lake la kaskazini kutoka mikononi mwa wanamgambo hao. Marekani na Umoja wa Mataifa wanataka tahadhari zaidi ichukuliwe kukabiliana na wanamgambo hao.
Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE
Mhariri:Josephat Charo