1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Mkuu Abdullah al-Thinni wa Libya ''ajiuzulu''

12 Agosti 2015

Waziri Mkuu wa Serikali ya Libya inayotambuliwa kimataifa Abdullah al-Thinni amesema kupitia televisheni kuwa anajiuzulu, lakini msemaji wa serikali ya nchi hiyo amesema waziri mkuu huyo ameeleweka vibaya.

https://p.dw.com/p/1GDkn
Waziri Mkuu wa Libya aliyejiuzulu, Abdullah al-Thinni
Waziri Mkuu wa Libya aliyejiuzulu, Abdullah al-ThinniPicha: picture-alliance/AP Photo/A. Zemlianichenko

Kauli ya Waziri Mkuu Abdullah al-Thinni ameitoa katika mahojiano na kituo kimoja cha televisheni nchini mwake. Baada ya maswali mengi makali kutoka kwa wananchi wenye hasira, waziri mkuu huyo amesema atajiuzulu kwa moyo safi.

''Nilitekeleza majukumu yangu na roho yangu hainisuti, na ninasema samahani ikiwa nilifanya makosa. Vile vile naomba kila mmoja kuniondolea majukumu haya, na kuanzia Jumapili nitawasilisha rasmi barua yangu ya kujiuzulu''. Amesema al-Thinni.

Hata hivyo, katika ishara dhahiri ya nchi inayopita katika msukosuko, msemaji wa serikali ya Libya Hatemi al-Arabi ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba al-Thinni hataondoka madarakani, na kwamba watu wamemwelewa vibaya. Al-Arabi amesema alichomaanisha al-Thinni, ni kwamba atajiuzulu tu ikiwa wananchi wake watasema hawamtaki.

Maswali makali ya raia wenye hasira

Katika mahojiano hayo kwa njia ya televisheni, Abdullah al-Thinni alikuwa ameulizwa maswali makali na wananchi wenye hasira, ambao waliishutumu serikali yake kushindwa kuwapatia huduma za msingi kama vile umeme, na kuhakikisha usalama katika maeneo inayoyadhibiti.

Mzozo wa Libya unayahusisha makundi kadhaa ya yenye silaha
Mzozo wa Libya unayahusisha makundi kadhaa ya yenye silahaPicha: picture-alliance/dpa/Str

''Kama kuondoka kwangu ndio suluhisho la matatizo hayo, natangaza hapa hapa kwamba nitawasilisha barua yangu ya kujiuzulu mbele ya bunge Jumapili'', amesema al-Thanni. Katika mahojiano hayo ya jana usiku, waziri mkuu huyo alikosolewa pia kwa kushindwa kukomesha rushwa katika serikali yake.

Serikali ya kuchaguliwa anayoiongoza Abdullah al-Thinni ina makao yake katika mji mdogo wa Tobruk ulio mashariki mwa Libya, tangu mwaka jana ilipoupoteza mji mkuu Tripoli kwa makundi ya wanamgambo wa kiislamu. Mwezi Mei alinusurika jaribio la kumuuwa, baada ya watu wenye silaha kulifyatulia risasi gari lake baada ya mkutano bungeni.

Mazungungumzo ya amani yanayosuasua

Mapema jana makundi yanayohasimiana nchini Libya yalikuwa yameanza mazungumzo mjini Geneva, ambayo yanalenga kutafuta muafaka wa kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa. Wawakilishi wa kundi lenye nguvu linaloudhibiti mji mkuu Tripoli walijiunga na duru hiyo ya mazungumzo yanayodhaminiwa na Umoja wa Mataifa, baada ya kuyasusia mwezi uliopita.

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Libya, Bernardino Leon
Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Libya, Bernardino LeonPicha: picture-alliance/dpa/S. Di Nolfi

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Libya Bernardino Leon ambaye anayaendesha mazungumzo hayo ya Geneva, ameyataka makundi muhimu kukubaliana kuunda serikali ya umoja wa kitaifa, kwa matumaini kwamba inaweza kuleta amani ya kudumu nchini Libya.

Makubaliano ya amani ya mpito yalifikiwa mwezi uliopita yakiwa na lengo la kurejesha utulivu nchini Libya, lakini yalipingwa na kundi lenye nguvu linaliudhibiti mji mkuu, Tripoli, ambalo lilisema hayaridhishi.

Libya ambayo ilitumbukia katika mzozo baada ya kuangushwa kwa utawala wa muda mrefu wa kanali Moamar Gaddafi mwaka 2011, hivi sasa inayo mabunge mawili yanayogombania madaraka, na makundi kadhaa ya wanamgambo wenye silaha, wanaowania udhibiti wa raslimali katika taifa hilo la Afrika Kaskazini linalozalisha mafuta kwa wingi.

Mwandishi: Daniel Gakuba/dpae/afpe

Mhariri: Iddi Ssessanga